DKT. SAMIA AAHIDI KUIFANYA KIGOMA KUWA KITOVU CHA BIASHARA NA UCHUMI
Kigoma - Mgombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, amehitimisha duru ya kwanza ya kampeni zake katika mkoa wa Kigoma kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Jimbo la Kigoma Mjini.
Licha ya mkutano huo kufanyika majira ya asubuhi, mamia kwa maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Kigoma Ujiji walijitokeza kumsikiliza, ambapo aliwasilisha sera na mipango ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano ijayo endapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza pamoja na wagombea wengine wa chama hicho katika nafasi za ubunge na udiwani.
Kigoma Kitovu cha Biashara na Uchumi
Akihutubia wananchi, Dkt. Samia alisisitiza dhamira ya serikali kuufanya mkoa wa Kigoma kitovu cha biashara na uchumi wa kikanda.
“Enzi za Kigoma kuitwa mwisho wa reli zimekwisha. Kwa kasi ya maendeleo ya sasa, Kigoma inajengeka kuwa kitovu cha biashara na uchumi wa kikanda,” alisema.
Alibainisha kuwa mradi wa reli ya kisasa (SGR) hauishii Kigoma pekee, bali unasonga mbele kuunganisha Tanzania na Burundi pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Aidha, alikumbusha miradi aliyozindua mwaka 2022 katika maeneo ya Kakonko na Kibondo ikiwemo barabara ya Kabingo–Nyakanazi, miradi ya maji na hospitali ya wilaya, akiahidi kuendeleza kazi hiyo.
Miundombinu ya Usafiri na Usafirishaji
Dkt. Samia aliwataka wananchi kuendelea kuiamini CCM ili kukamilisha mpango wa kuifanya Kigoma kitovu cha uchukuzi. Alifafanua kuwa serikali inaendelea kuboresha uwanja wa ndege wa Kigoma na kuliongezea nguvu Shirika la Ndege la Taifa (ATCL).
Kuhusu reli, alisema mradi wa SGR kipande cha Tabora–Kigoma na Uvinza–Msongati (Burundi) unaendelea, huku vipande vya Dar es Salaam–Morogoro–Dodoma vikiwa vimekamilika. Serikali pia imenunua vichwa vitatu vipya vya treni, mabehewa 22 ya abiria na 44 ya mizigo, sambamba na ukarabati wa mabehewa zaidi ya 350 ya mizigo na 33 ya abiria.
Kwa upande wa usafiri wa majini, Dkt. Samia aliahidi uboreshaji wa bandari za Ujiji, Kibirizi na Kabwe. Aidha, alisema ujenzi wa meli nne katika Bandari ya Kalema unaendelea ambapo moja imekamilika na tatu zipo hatua za mwisho, huku ukarabati wa meli kongwe ukiendelea. Pia, shipyard ya Katabe inajenga meli mbili za mizigo ikiwemo moja yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 ambayo itapokea shehena kutoka SGR.
Ujenzi wa Barabara na Madaraja
Mgombea huyo wa CCM alisisitiza dhamira ya serikali kuhakikisha barabara na madaraja yote muhimu katika mkoa huo yanakamilika, ikiwemo kipande cha barabara ya Manyovu kuelekea mpakani. Aliongeza kuwa barabara za vijijini ambazo hazipo kwenye mpango wa lami zitajengwa kwa changarawe ili ziweze kupitika kwa urahisi.
Nishati na Uwekezaji
Kuhusu sekta ya nishati, Dkt. Samia alieleza kuwa serikali imefanikisha kuunganisha vijiji na mitaa mingi mkoani Kigoma katika kipindi cha miaka minne. Aliwaahidi wananchi kuwa katika kipindi kijacho, serikali yake itakamilisha mradi wa kuzalisha megawati 46 za umeme katika Mto Malagarasi kupitia kituo cha Kidagwe, ambacho kitawezesha mkoa mzima kupata nishati ya uhakika.
Alisisitiza kuwa upatikanaji wa nishati utavutia wawekezaji, akitoa mfano wa Kiwanda cha Sukari cha Kasulu ambacho tayari kimeajiri vijana 500 na kuchangia kupunguza bei ya sukari nchini. Pia, alibainisha kuwepo kwa kiwanda cha saruji na mipango ya ujenzi wa konga za viwanda vitakavyowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.
Kwa ujumla, Dkt. Samia aliwaomba wananchi wa Kigoma kumpa ridhaa ya kuendelea kuongoza ili kutimiza mipango ya maendeleo ya CCM na kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara, uchumi na uchukuzi katika ukanda wa Maziwa Makuu.









