Breaking News

INEC YASITISHA UCHAGUZI JIMBO LA FUONI KUFUATIA KIFO CHA MGOMBEA WA CCM JIMBO HILO

Zanzibar — Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesitisha uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Fuoni, Wilaya ya Magharibi B, Zanzibar kufuatia kifo cha mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abass Ali Mwinyi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Miraji Mwadini Haji, kusitishwa huko kumetokana na taarifa rasmi iliyowasilishwa kwa Tume na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar kwa barua yenye Kumb. Na. CCM/AKZ/U30/22/VOL XIV/109 ya tarehe 25 Septemba 2025.

Kwa mujibu wa kifungu cha 71 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, Tume itapanga tarehe mpya ya uteuzi wa wagombea na kuanzisha upya mchakato wa uchaguzi katika jimbo hilo, kwa notisi itakayotolewa kupitia Gazeti la Serikali.

Msimamizi wa Uchaguzi ameeleza kuwa wagombea waliokwishaidhinishwa awali wataendelea kubaki kwenye orodha, isipokuwa iwapo mgombea atajitoa, na kusisitiza kwamba hakutakuwa na kampeni zozote za ubunge katika Jimbo la Fuoni mpaka mgombea mpya atakapoteuliwa.