DC MKUDE AAHIDI MIKOPO NAFUU KWA MAFUNDI GEREJI NA WAFANYABIASHARA WA MLIMA SUYE, ARUSHA
Na Woinde Shizza, Arusha - Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ameahidi kuwasaidia mafundi gereji na wafanyabiashara wa eneo la Mlima Suye kupata mikopo yenye riba nafuu kupitia Halmashauri ya Jiji la Arusha, ili kuwawezesha kuinua shughuli zao za kiuchumi.
Akizungumza leo jijini Arusha katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi wa Kata ya Kimandolu, Mkude alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuwainua wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya masharti nafuu.
“Ndugu mafundi gereji nimewasikia vizuri. Mnahitaji mikopo ili mjiongeze kwenye kazi zenu. Naahidi baada ya uchaguzi, nitahakikisha afisa husika anakuja hapa kuzungumza nanyi ili muweze kujua hatua sahihi za kufuata ili kufikia malengo yenu,” alisema Mkude.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara wa eneo hilo kuhakikisha wanalinda na kutunza mazingira, akisema mazingira safi yanachangia kuvutia wateja na kuboresha afya za wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Mafundi Gereji wa Krokoni Suye, James Agustoni, alisema mafundi hao wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ubovu wa miundombinu na ukosefu wa hati miliki ya eneo wanalofanyia kazi.
“Tulianzia Krokoni kabla ya kuhamishiwa hapa Suye, lakini tatizo kubwa ni miundombinu mibovu. Wakati wa mvua, eneo hili huwa hatarishi kwa sababu ya mafuriko. Tunaomba serikali itusaidie,” alisema Agustoni.
Naye Mwenyekiti Msaidizi wa umoja huo ambaye pia ni mmiliki wa Nelson Shop, Nelson Natai, alisema iwapo miundombinu itaboreshwa, itawawezesha mafundi na wafanyabiashara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Miundombinu bora itarahisisha wateja kufika bila changamoto. Hilo litasaidia kukuza biashara na kuongeza mapato kwa mafundi,” alisema Natai.
Mkude alihitimisha kwa kuwataka mafundi na wafanyabiashara hao kudumisha umoja wao na kufuata taratibu za kisheria ili waweze kunufaika ipasavyo na fursa za kifedha zinazotolewa na serikali.




