Breaking News

CWT: WANANCHI PUUZENI UPOTOSHAJI JUU YA USHIRIKI WA WALIMU UCHAGUZI MKUU

Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimekanusha taarifa zinazosambaa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari ikihamasisha walimu kutoshiriki kwenye shughuli za Uchaguzi Mkuu, ambapo baadhi ya walimu hutumika kama wasaidizi wa shughuli za uchaguzi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Chama kimetoa rai kwa walimu, wanachama wote na wananchi wote kwa ujumla kupuuza taarifa hizo kwani hazina ukweli wala msingi wowote na zinalenga kuleta taharuki, uzushi na uchonganisi ambao unapaswa kupingwa kwa nguvu zote ili kulinda umoja, amani na utulivu ambao ni tunu ya taifa letu.

Pia Chama kinapenda kuwahakikishia walimu, Serikali na wananchi wote kwa ujumla kuwa kitaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kuwa tabia hii ya utoaji taarifa potofu inakomeshwa ili kulinda misingi na madhumuni ya uwepo wa vyama vya wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria na kanuni za nchi.

Katika taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu Joseph Misalaba ,Chama kimewataka Walimu wote kuendelea na msimamo wa kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba, 2025 kwenda kupiga kura kwani ndio msimamo wa chama ambao ulikwisha tolewa na msemaji wa chama (ambaye ni rais wa CWT).

Taarifa hiyo ilisisitiza walimu na umma kwa ujumla kuwa mabalozi wazuri wa upendo, amani, umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo thabiti ya taifa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadae.

Aidha chama hichoi kimeishukuru serikali kwa kuendelea kutatua kero mbalimbali za walimu kwa kushirikiana na chama cha walimu Tanzania (CWT).