MCT, UWEZO TANZANIA KUSHIRIKIANA KUIMARISHA UANDISHI WA HABARI ZA ELIMU
Baraza la Habari Tanzania (MCT) na UWEZO Tanzania wameingia makubaliano ya ushirikiano yatakayowawezesha waandishi wa habari kuimarisha uandishi wa habari za elimu kwa weledi, ukijikita katika ushahidi na usawa wa kijinsia.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa UWEZO Tanzania, Baraka Mgohamwende.
Kwa mujibu wa pande hizo mbili, lengo kuu ni kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinazalisha taarifa bora na jumuishi zinazochangia mabadiliko chanya kwenye jamii kupitia elimu. Hii ni pamoja na kusisitiza umuhimu wa kusikiliza na kuibua sauti za wasichana, wanafunzi walioko katika mazingira magumu, na makundi mengine yaliyotengwa.
“Mkataba huu ni hatua muhimu katika kuimarisha nafasi ya uandishi wa habari za elimu nchini, ili kuhakikisha elimu inajadiliwa kwa kina na kwa kuzingatia usawa,” alisema Sungura.
Kwa upande wake, Mgohamwende alisisitiza kuwa taarifa sahihi na zenye ushahidi zitasaidia jamii kutambua changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya elimu, na hivyo kuchochea maboresho endelevu.
Hafla ya utiaji saini ilishuhudiwa na Greyson Mgoi, Mkuu wa Mawasiliano wa UWEZO Tanzania, pamoja na Josephat Mwanzi, Meneja wa Programu wa MCT.









