DKT. SAMIA: DEMOKRASIA HAIPIMWI KWA USHINDI, BALI KWA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amegusa mioyo ya Watanzania kwa kusisitiza falsafa ya Umoja wa Kitaifa, maridhiano, na kuheshimu kila sauti.
Akizungumza mbele ya viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, baada ya kuapishwa jana Rais Samia alieleza bayana kuwa: “Demokrasia haipimwi kwa nani kashinda uchaguzi, bali kwa jinsi tunavyoendesha mambo yetu baada ya uchaguzi.”
Rais Samia alitumia jukwaa hili kuwashukuru wagombea wengine 17 waliowania nafasi ya Urais , akipongeza ukomavu wa kidemokrasia uliojitokeza wakati wa kampeni. Alisisitiza kuwa uchaguzi umekwisha, na sasa jukumu lililo mbele yao wote ni kufanya kazi ya kulijenga Taifa na Utu wa Mtanzania.
Akisisitiza umuhimu wa mazungumzo, Rais alionya wale wote waliochochea uvunjifu wa amani, akisema: "Vurugu na uvunjifu wa amani huishia kupimana nguvu... ila mazungumzo huzaa mshikamano." Aliwahimiza Watanzania kuchagua hekima badala ya ghadhabu, na amani badala ya vurugu.
Akirejea falsafa ya 4R's (Reconciliation, Resilience, Reforms, Re Construction/Building), Mhe. Rais Samia ameahidi kulitumikia Taifa kwa nguvu zote, vipawa vyote, na maarifa yote. Aliongeza kuwa Serikali yake itaendelea kusimamia yote yanayohusu kujenga Umoja na Mshikamano wa Taifa.
Alibainisha kuwa utekelezaji wa kina wa dhana ya Kazi na Utu na mwelekeo wa Serikali kwa miaka mitano ijayo utatolewa rasmi katika Hotuba ya Uzinduzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha Rais alizishukuru Jumuiya za Kimataifa na Kikanda, ikiwemo SADC, AU, na EAC, kwa kuleta waangalizi. Akikiri kupokea maoni yao kwa heshima kubwa , alisisitiza msimamo wa Taifa kwa kunukuu kauli ya Hayati Benjamin Mkapa: "Maagizo yao tumeyakataa, ushauri wao tutauzingatia ili tufanye vizuri zaidi siku zijazo."




