Breaking News

MCT YAWAITA WADAU KUTATHMINI MATUKIO YA UCHAGUZI

Na Mwandishi wetu - Kufuatia matukio ya ghasia na changamoto zilizojitokeza baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Baraza la Habari Tanzania (MCT) linafanya mchakato wa kukutana na wadau wote wa habari kwa lengo la kulinda mustakabali wa uhuru wa habari na utawala bora nchini Tanzania.

Taasisi ambazo Baraza itafanya mashauriano nayo ni pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Bodi ya Kuwatambua Waandishi wa Habari (JAB), Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Mashirika ya Kiraia (CSOs), na mashirika ya habari chini ya Muungano wa Haki ya Kupata Habari (CoRI).

Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza iliyosainiwa na Katibu Mtendaji wake Ernest Sungura,lengo kuu la mashauriano haya ni kutambua mikakati thabiti ya kulinda uhuru wa habari, kutetea haki ya wananchi kutoa maoni, na kuimarisha utawala wa kidemokrasia Tanzania.

Oktoba 29,2025, Watanzania walishiriki katika uchaguzi wa Rais, Wabunge, Madiwani, na masheha kwa upande wa Zanzibar. Hata hivyo, kile kilichopaswa kuwa wakati wa kusherehekea demokrasia, kiliingiliwa na matukio ya vurugu yaliyoishtua nchi na kuvuta macho ya dunia.

Kwa mujibu wa MCT matukio hayo yametikisa sana sifa ya nchi ya kuwa ya amani, umoja, na mshikamano wa kijamii. Pia yameibua wasiwasi mkubwa kuhusu mwelekeo wa Tanzania kuelekea uwazi, uwajibikaji, na utawala bora, ambazo ni nguzo za msingi za demokrasia yenye mafanikio.

Taarifa hiyo ilisema kwamba kabla ya uchaguzi, MCT ilitoa Mwongozo kamili na kutoa wito kwa wadau wote, ikiwemo taasisi za serikali, maofisa wa uchaguzi, vyombo vya ulinzi, na wananchi, kutambua jukumu muhimu la vyombo vya habari , utawala wa sheria na maadili ya kitaaluma.

Hata hivyo, vurugu zilizotokea zimeacha taifa likihoji kama kila mdau alitimiza majukumu yake kwa uaminifu na bidii