MPAKA WA TANZANIA NA KENYA NI SALAMA - RC MAKALLA
# Aridhishwa na usalama na ufanyaji biashara eneo la Namanga
# Aeleza umuhimu wa Mpaka huo kibiashara na ustawi wa Jamii
Na mwandishi wetu - Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla ameeleza kuridhishwa na hali ya ulinzi na usalama katika Mpaka wa Namanga unaounganisha Mataifa ya Tanzania na Kenya kupitia Mkoa wa Arusha, akiwashukuru watendaji wa Pande zote mbili wanaofanya kazi kwenye Kituo cha pamoja cha forodha Namanga kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa pande zote.
Mhe. Makalla amebainisha hayo leo Alhamisi Novemba 06, 2025 Mjini Namanga wakati alipoambatana na Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa kwaajili ya kukagua hali ya Ulinzi na usalama katika eneo hilo pamoja na kuangazia ufanyaji wa biashara katika eneo hilo mara baada ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka shughuli zote za Kijamii na kiuchumi kuendelea katika maeneo mbalimbali nchini mara baada ya uchaguzi Mkuu.
"Nithibitishe kuwa Mpaka wa Tanzania na Kenya ni salama na kituo cha pamoja cha forodha Namanga kipo salama. Kituo hiki ni muhimu kwa nchi zetu zote mbili na kwa wananchi hususani hawa wa Mpakani kwani wao pia ni wanufaika wa moja kwa moja na fursa za kiuchumi na biashara kwahiyo ni muhimu kuendelea kueneza amani, umoja na mshikamano kwenye mpaka huu kwani sote ni wanufaika." Amesema Mhe. Makalla.
CPA Makalla kadhalika amewapongeza Viongozi na watendaji wa kituo hicho cha forodha ka kuendelea kuimarisha mahusiano na kukuza biashara katika eneo hilo suala ambalo limekifanya Kituo hicho pia kuwa eneo muhimu la mabadilishano ya bidhaa kati ya Tanzania na Kenya, akisema kutetereka kwa Mpaka huo kuna athari kubwa kwa uchumi wa nchi hizo na ustawi wa jamii.
Kwa Upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato nchini Kenya (KRA) kwenye Kituo hicho cha Namanga Bw. Nicholous Mugambi amemuhakikishia CPA Makalla kuwa wataendelea kushirikiana na Mamlaka za Tanzania katika kukuza mahusiano na biashara miongoni mwa nchi hizo mbili, akisisitiza umuhimu wa amani kama msingi wa kufikia mafanikio katika biashara na ustawi wa wananchi wa Tanzania na Kenya.









