RAIS DKT. MWINYI ATANGAZA BARAZA LA MAWAZIRI, AZITANGAZA WIZARA 20 KATIKA AWAMU YA PILI YA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
Na Mwandishi wetu, Zanzibar - Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza uteuzi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri wateule wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akibainisha kuwa uteuzi huo unalenga kuongeza kasi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.
Akizungumza leo tarehe 13 Novemba 2025 katika hafla iliyofanyika Ikulu Zanzibar, Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya Nane, katika kipindi chake cha pili, itakuwa na jumla ya Wizara 20 badala ya 18 zilizokuwepo awali, hatua aliyoeleza inalenga kuimarisha usimamizi wa sekta mbalimbali za Serikali.
Hafla hiyo imehudhuriwa na waandishi wa habari na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ametangaza majina ya Mawaziri wateule kama ifuatavyo:
MAWAZIRI
1. Dkt. Haroun Ali Suleiman – Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora
2. Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum – Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu
3. Mhe. Dkt. Juma Malik Akil – Waziri wa Fedha na Mipango
4. Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa – Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ
5. Mhe. Shariff Ali Shariff – Waziri wa Kazi na Uwekezaji
6. Mhe. Hamza Hassan Juma – Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi
7. Mhe. Rahma Kassim Ali – Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi
8. Mhe. Lela Mohamed Mussa – Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
9. Mhe. Shaaban Ali Othman – Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji
10. Mhe. Suleiman Masoud Makame – Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo
11. Mhe. Nadir AbdulLatif Alwardy – Waziri wa Maji, Nishati na Madini
12. Mhe. Masoud Ali Mohamed – Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi
13. Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed – Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi
14. Mhe. Anna Athanas Paul – Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
15. Mhe. Mudrik Ramadhan Sdraga – Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu
16. Mhe. Riziki Pembe Juma – Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo
NAIBU MAWAZIRI
1. Mhe. Badria Atai Masoud – Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi
2. Mhe. Dkt. Hamad Omar Bakari – Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
3. Mhe. Ali AbdulGullam Hussein – Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo
4. Mhe. Zawadi Amour Nassor – Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
5. Mhe. Salha Mohamed Mwinjuma – Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi
6. Mhe. Seif Kombo Pandu – Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini
7. Mhe. Dkt. Salum Soud Hamid – Naibu Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo
8. Mhe. Mboja Ramadhan Mshenga – Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi
9. Mhe. Mohamed Suamini Mohamed – Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu
10. Mhe. Hassan Khamis Hafidh – Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji
11. Mhe. Khadija Salum Ali – Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa nafasi za Wizara nne bado ziko wazi hadi pale Serikali itakapokamilisha makubaliano na Chama cha ACT Wazalendo kuhusu uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Wizara zilizoachwa wazi ni:
1. Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
2. Wizara ya Afya
3. Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale
4. Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda
Rais Mwinyi amesisitiza kuwa uteuzi huo umezingatia uwiano wa kijinsia, uwakilishi wa pande zote mbili za Unguja na Pemba, pamoja na uzoefu wa viongozi katika sekta zao.
Ameongeza kuwa Serikali inaingia katika zama za uchumi wa kidijitali, hivyo itaendelea kuwekeza katika teknolojia, mifumo ya kisasa na ubunifu ili kuongeza kasi ya maendeleo.
Aidha, amesema Serikali itaweka mfumo wa tathmini ya utendaji kazi kwa viongozi wote, ili kuhakikisha uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mawaziri na Naibu Mawaziri hao wateule wanatarajiwa kuapishwa siku ya Jumamosi, tarehe 15 Novemba 2025, saa 8:00 mchana, Ikulu Zanzibar.




