SIKU YA WATOTO DUNIANI: UBALOZI WA PALESTINA WAONYA KUHUSU KUONGEZEKA KWA MATESO YA WATOTO CHINI YA UKOLONI WA KIJESHI WA ISRAELI
Dar es Salaam — Katika kuadhimisha Siku ya Watoto Duniani, Ubalozi wa Palestina nchini Tanzania umeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kukomesha kile ilichokiita “mateso ya muda mrefu na ukiukaji mkubwa wa haki za watoto nchini Palestina” unaofanywa chini ya utawala wa kijeshi wa Israeli.
Kwa miongo kadhaa, watoto wa Palestina wameripotiwa kukumbana na vifo, ulemavu wa kudumu, uharibifu wa nyumba na shule, ukosefu wa huduma muhimu, na mazingira ya hofu yanayotokana na mashambulizi ya kijeshi na ukatili wa walowezi. Ubalozi unasema hali hizi zimeathiri ukuaji na ustawi wao kwa kiwango kikubwa.
Katika taarifa hiyo, ubalozi unasema kwamba tangu kuanza kwa kile inachoeleza kama “mashambulizi ya kigaidi ya Israeli dhidi ya Gaza,” eneo hilo limeendelea kushuhudia vifo vingi, uharibifu mkubwa wa miundombinu, na uhamisho wa raia waliokosa hifadhi salama. Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Yerusalemu Mashariki, nao umeripotiwa kushuhudia ongezeko la vifo vya watoto, vizuizi vya harakati, uvamizi wa mara kwa mara wa kijeshi, na ukatili wa walowezi.
Takwimu Zinazotia Huzuni (2023–2025)
Watoto 18,592 wako miongoni mwa zaidi ya 69,483 waliouawa Gaza.
Zaidi ya watu 170,000 wamejeruhiwa, 70% wakiwa wanawake na watoto.
Takribani watoto 40,000 wamebaki yatima.
Mamia ya maelfu wanaishi na ulemavu au majeraha makubwa bila kupata matibabu ya kutosha.
Huduma za afya, ustawi wa watoto na msaada wa kisaikolojia zimeporomoka vibaya.
Ukingo wa Magharibi umeona mauaji ya watoto 210 tangu 7 Oktoba 2025, huku watoto 350 wakiripotiwa kuzuiliwa katika vituo vya Israeli, wengi bila mashtaka rasmi.
Ubalozi unasema kwamba zaidi ya miaka 18 ya kizuizi cha ardhini, baharini na angani dhidi ya Gaza kimejitokeza kama chanzo kikuu cha uhaba wa dawa, chakula, umeme na maji safi kwa zaidi ya wakazi milioni 2.3 nusu yao wakiwa ni watoto.
Msingi wa Kisheria
Taarifa inakumbusha kuwa chini ya Mkataba wa Geneva wa Nne na Mkataba wa Haki za Mtoto (CRC), Israeli inawajibika kulinda raia, hususan watoto, na kujiepusha na adhabu za pamoja, uhamisho wa kulazimishwa, mauaji yasiyo halali, na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia. Ukiukaji wa masharti hayo, kwa mujibu wa ubalozi, unaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.
Wito kwa Jumuiya ya Kimataifa
Serikali ya Palestina inazitaka taasisi za kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa:
1. Kujumuisha jeshi la Israeli kwenye “orodha ya aibu” ya wahalifu wa haki za watoto.
2. Kuzuia mashambulizi yanayolenga raia na watoto kwa kuchukua hatua za haraka.
3. Kuhakikisha ufikiaji salama na usio na vikwazo kwa shule, hospitali, makazi na huduma za kisaikolojia.
4. Kuwaachia watoto wanaoshikiliwa kiharamu katika vituo vya Israeli.
5. Kuilazimisha Israeli kuheshimu sheria za kimataifa, ikiwemo maoni ya ICJ ya 2024 kuhusu Palestina.
6. Kuwekeza katika mipango ya kurejesha afya, elimu na afya ya akili kwa watoto wa Palestina.
7. Kuchukua hatua za kidiplomasia na kiuchumi ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria za kimataifa.
Ubalozi wa Palestina unasisitiza kuwa kila mtoto ana haki ya kuishi, kulindwa, kupata elimu, na kukua katika mazingira salama haki ambazo unasema zinaendelea kukandamizwa kwa watoto wa Palestina.




