TLS KUWAPA MSAADA WA KISHERIA WATUHUMIWA WA MASHAURI YA JINAI NCHINI
Na Neema Mpaka, Dar es Salaam - Mawakili WanaChama wa chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wameahidi kuwasaidia kutoa haki ya msaada wa kisheria kuhusu mwenendo wa mashauri ya jinai yanayoendelea kufunguliwa kote nchini hususani ndugu na wazazi wanaotuhumiwa katika mashauri ya makosa hayo.
Wapo watu wanashikiliwa katika vituo vya polisi kabla ya uchaguzi Mkuu huku ndugu zao wakiwa hawajui walipo ambapo kutokana na sintofahamu iliyopo, wapo wanaoamini kwamba huenda ndugu zao wamekwisha fariki hata mawakili kupata wakati mgumu kuonana na wateja wao katika vituo na wakati mwingine kunyimwa haki kuonana na wateja wanaoshikiliwa katika vituo vya polisi nchini.
Hayo yamesemwa leo Novemba 11 2025 Jijini Dar es Salaam wakati mawakili hao wakielezea mbele ya waandishi wa habari mwenendo wa mashauri ya jinai yanayoendelea kufunguliwa kote nchini.
"Watuhumiwa wengi wa makosa haya ni vijana wenye umri kati ya miaka 19 mpaka 25 baada ya mashauri haya kuanza kufunguliwa tulikaa na kufanya tathimini ambapo tulibaini kuwa watuhumiwa walio wengi uelewa wao wa kisheria ni mdogo na wengine hawana hata uwezo wa kulipia gharama za mawakili kwa ajili ya kuwawakilisha," amesema mmoja wa mawakili hao William Maduhu.
Maduhu akielezea haki ya msaada wa kisheria kwa watuhumiwa wote hususani ndugu na wazazi wa wanaotuhumiwa katika mashauri hayo wamesema Novemba 7 , 2025 mashauri yanayohusisha kula njama ya kufanya kosa la jinai, uhaini, uharibifu wa Mali, unyang'anyi wa kutumia silaha, uchomaji wa mali na kufanya maandamano bila vibali yalifunguliwa na Jamhuri.
TLS imesema idadi ya watuhumiwa waliokuwa wanashikiliwa katika mahabusu mbali mbali kote nchini inakadiliwa kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam pekee zaidi ya watu 400 walikamatwa,Mkoa wa Mwanza watu zaidi ya 200 walikamatwa, Kilimanjaro takribani watu 312 walikamatwa ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro watuhumiwa 300 wamekwisha achiwa na 12 bado wanashikiliwa.
Maduhu amesema kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 wao mawakili kutoka TLS wameamua kujitolea kutoa msaada wa kisheria ikiwemo kuwawakilisha mahakamani watuhumiwa wote waliofikishwa mahakamani tangu tarehe 7 na ambao wataendelea kufikishwa mahakamani siku Hadi siku bila malipo na bila masharti yoyote.
Mawakili hao wameelezea Dar es Salaam pekee watuhumiwa zaidi ya 400 walikamatwa ambapo 240 wamefikishwa mahakamani na wengine bado wanaendelea kushikiliwa kinyume na sheri na wengine wameachiwa ingawa hakuna idadi kamili.
Wameelezea kuwa kwa wazazi wa Dar es Salaam wawatembelee watoto wao katika gereza la Segerea na walioko katika mikoa mingine wawatembelee katika Magereza yaliyoko Mkoa husika.
Vile vile Ndugu wametakiwa kuwa na vitambulisho wanapotembelea katika Magereza husika.
Kwa upande wake wakili Paulo Kisabo amesema kuwa wao kama mawakili wanatoa uwakilishi wa kisheria kwa watuhumiwa kote nchini bila ubaguzi.
"Tunatoa wito kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini kutumia Mamlaka yake kisheria kufuta hizo kesi kwani kwa tathmini yetu tunaona mashtaka yaliyofunguliwa hayana msingi wa kisheria,"amesema Wakili Kisabo.




