Breaking News

SIMBACHAWENE AWATAKA NIDA KUCHAPA KAZI, KUMUUNGA MKONO RAIS

Na Mwandishi Wetu, NIDA - Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (Mb), ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na weledi ili kumuunga mkono Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza ajenda ya maendeleo ya Taifa katika kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.
 
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo alipotembelea Ofisi za Makao Makuu ya NIDA jijini Dar es Salaam, Disemba 18, 2025 ambapo alipata fursa ya kukagua shughuli mbalimbali za usajili na utambuzi wa wananchi, pamoja na mifumo inayotumika katika utoaji wa huduma.
Katika ziara hiyo, Simbachawene amesema NIDA ina jukumu nyeti katika kuhakikisha wananchi wote wanatambuliwa rasmi, hatua inayosaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu, kupunguza wizi na udanganyifu, sambamba na kuimarisha hali ya usalama wa nchi.
 
Amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, kwa maboresho aliyoyafanya katika kuimarisha utendaji kazi wa NIDA, hususan katika kuboresha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza ufanisi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati.
Amesema huduma ya usajili na utambuzi wa wananchi ni muhimu katika dunia ya sasa ya kidijitali, kwani mifumo mingi ya kisasa inahitaji utambulisho wa uhakika ili kuwezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Kupitia Utambulisho wa Taifa, wananchi wanawezeshwa kupata huduma muhimu ikiwemo huduma za kifedha, huduma za afya, elimu pamoja na huduma nyingine za kijamii.
 
Pia amewahimiza watumishi wa NIDA kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Maadili ya Utumishi wa Umma. Amewasisitiza kuwa kazi yao ni mhimili muhimu wa ujenzi wa Taifa salama, lenye maendeleo na linaloendana na mabadiliko ya kidijitali.