Breaking News

TBN YAIPONGEZA TANZANIA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 64 YA UHURU

Dar es Salaam, Desemba 9 Tanzania Bloggers Network (TBN) imetoa salamu za pongezi kwa Watanzania wote katika kuadhimisha miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania, ikiendelea kusisitiza umuhimu wa amani, utulivu na mshikamano kama nguzo za maendeleo ya Taifa.

Kupitia taarifa yake, TBN imelitumia tukio hili muhimu kuwakumbusha Watanzania kutafakari safari ya Taifa tangu kupata Uhuru, mafanikio yaliyofikiwa na wajibu wa kizazi cha sasa katika kuendeleza jitihada za waasisi wa Taifa.

Taarifa hiyo imeyanukuu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kusisitiza kuwa Uhuru hauwezi kuwa kamili bila kujitegemea:
“Uhuru hauwezi kukamilika pasipo kujitegemea. Hatuwezi kuitwa huru kama tunategemea wengine kutupatia mahitaji yetu ya kimsingi.”

TBN imesisitiza kuwa mitandao ya kijamii inapaswa kuwa chombo cha kuunga mkono juhudi za ujenzi wa Taifa badala ya kueneza mifarakano. Imenukuu pia kauli ya Rais mstaafu Benjamin William Mkapa aliyewahi kusema kwamba amani si jambo la kutokea lenyewe, bali ni kitu kinachohitaji kulindwa kila siku ili maendeleo yawezekane.

Kadhalika, TBN imekumbusha mchango wa viongozi mbalimbali katika safari ya Tanzania, ikimnukuu Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyewahi kusema kuwa “Kila utawala na zama zake, kila kiongozi na mchango wake katika ujenzi wa Taifa.”

Katika kipindi hiki ambacho nchi ipo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, taarifa ya TBN imeeleza kuwa Watanzania wanapaswa kuunga mkono mwelekeo wa 4R Maridhiano, Uvumilivu, Mageuzi na Kujenga upya kama njia ya kuimarisha umoja na kuchochea maendeleo.

Aidha, TBN imewahimiza Watanzania kutumia uhuru wa maoni kwa kujenga Taifa, si kulibomoa, huku ikiwataka kuendelea kuthamini amani, kufanya kazi kwa bidii na kuepuka kuwa sehemu ya uchochezi unaoweza kudhoofisha mafanikio ya miaka 64 ya Uhuru.

“Tanzania Kwanza, Kazi na Utu Tusonge Mbele,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe.