Breaking News

ACT WAZALENDO YAKUMBUKA MIAKA 25 TANGU YA TUKIO LA JANUARY 26 NA 27 2001, YATOA WITO WA HAKI NA MAGEUZI YA KITAIFA

Zanzibar - Chama cha ACT Wazalendo kimeungana na Wazanzibar pamoja na wapenda haki duniani kuadhimisha miaka 25 tangu kutokea kwa matukio ya kusikitisha ya Januari 26 na 27, 2001, yanayofahamika kama Januari ya Damu, kikisisitiza umuhimu wa haki, utu wa binadamu na mageuzi ya kudumu ya kitaasisi ili kuzuia kurejea kwa ukatili wa kisiasa.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa leo, chama hicho kimeeleza kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya tafakari nzito juu ya thamani ya maisha ya Wazanzibar na madhara makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyotokea katika kipindi hicho.

ACT Wazalendo kimetoa salamu za pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao, waliojeruhiwa na waliolazimika kukimbia makazi yao kufuatia machafuko ya mwaka 2001, kikieleza kuwa heshima bora kwa wahanga hao ni kuhakikisha Zanzibar hairudii tena historia ya giza la umwagaji damu.

Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kusikitishwa na muendelezo wa vitendo vya ukatili dhidi ya raia, kikitolea mfano matukio ya Oktoba 29 na 30, 2025, ambapo baadhi ya Watanzania walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa katika mazingira yanayodaiwa kuhusisha vyombo vya dola. Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, matukio hayo yanaonesha kuwa taifa bado halijajifunza kikamilifu kutoka makosa ya Januari 2001.

Katika muktadha huo, chama hicho kimelaani vikali matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia na kudai uwajibikaji kwa wote waliohusika, kikisisitiza kuwa demokrasia haiwezi kujengwa juu ya hofu na mabavu.

ACT Wazalendo pia kimetoa wito kwa Serikali na wadau wa demokrasia kufanya mageuzi makubwa ya kisheria na kitaasisi, hususan katika mifumo ya uchaguzi na haki, ili kuhakikisha matakwa ya wananchi yanaheshimiwa na kuondoa mianya inayoruhusu matumizi mabaya ya nguvu za dola.

Aidha, chama hicho kimevitahadharisha vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Tume ya Uchaguzi kuhusu wajibu wao wa kikatiba, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linapitia mkwamo wa kisiasa kufuatia Uchaguzi wa Oktoba 2025. ACT Wazalendo kimesisitiza kuwa jukumu la taasisi hizo ni kulinda raia na haki zao, si kuzuia sauti za wananchi.

Kikihitimisha taarifa yake, ACT Wazalendo kimeeleza imani yake kuwa amani ya kweli haitokani na ukimya wa bunduki bali hutokana na haki, ukweli na kuheshimiwa kwa ridhaa ya wananchi, kikitoa wito kwa viongozi wote kuhakikisha kuwa suluhu ya mkwamo wa kisiasa wa sasa inajengwa juu ya misingi ya haki na maridhiano ya kweli.

“Tukumbuke yaliyopita ili tujenge yajayo kwa haki,” ilisisitiza taarifa hiyo