MAGEUZI BANDARI YA DAR: MAPATO YA SERIKALI YAPAA HADI TRILION 12.3, UFANISI WAONGEZEKA KWA 30%
Dar Es Salaam: Maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika Bandari ya Dar es Salaam yameongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi wa utendaji na mapato ya Serikali, hatua iliyoiimarisha Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema uwekezaji uliofanywa kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na kampuni za DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL) umeleta mageuzi makubwa ya kiutendaji na kifedha.
Msigwa alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia shehena tani milioni 27.7, sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na tani milioni 23.69 za mwaka 2023/2024. Aidha, katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2025, bandari hiyo ilihudumia tani milioni 16.7, ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Kutokana na kuimarika kwa ufanisi wa bandari, Msigwa alisema mapato ya Serikali yatokanayo na kodi za forodha yameongezeka hadi kufikia Shilingi trilioni 12.33 katika mwaka wa fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi trilioni 10.55 yaliyokusanywa mwaka 2023/2024.
“Maboresho haya yamepunguza muda wa meli kuhudumiwa kutoka wastani wa siku 30 hadi siku sita pekee kwa meli za makasha, hali iliyopunguza gharama za biashara na kuongeza mapato yatokanayo na ongezeko la mzunguko wa shehena,” alisema Msigwa.
Aidha, ushirikishwaji wa sekta binafsi kupitia DP World na TEAGTL umeiwezesha TPA kupunguza gharama za uendeshaji kwa wastani wa asilimia 57, jambo lililoimarisha uwiano wa faida ya mamlaka hiyo kutoka asilimia 66 hadi kufikia asilimia 78.
Msigwa aliongeza kuwa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa mhimili muhimu wa biashara za kikanda, ikihudumia nchi jirani zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Rwanda, Burundi, Malawi, Uganda na Zimbabwe, hali inayochangia ongezeko la mapato ya Serikali na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Alisisitiza kuwa kukamilika kwa miradi ya maboresho ya bandari kutaiwezesha Dar es Salaam kuhudumia meli kubwa za kisasa (Post Panamax), kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena hadi tani milioni 30 kwa mwaka na kuongeza zaidi mapato ya Serikali.





