NAIBU WAZIRI MILLYA ATETA NA BALOZI WA UTURUKI HAPA NCHINI
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Dkt. Bekir Gezer, Balozi wa Jamhuri ya Uturuki.
Mazungumzo hayo yalilenga kuendelea kumarisha ushirikiano wa kidiplomasia na uchumi kati ya Tanzania na Uturuki kupitia sekta mbalimbali ikiwemo elimu, kilimo, sayansi na teknolojia, afya, uchukuzi, ulinzi na usalama, biashara na uwekezaji, utalii na afya.
Balozi Mhe. Dkt. Gezer kubainisha kuwa pamoja na ukuaji mzuri wa biashara baina ya Tanzania na Uturuki, Nchi hizo zinapaswa kufikia lengo la pamoja lililowekwa wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyofanyika nchini Uturuki mwaka 2024 la kufikia rekodi ya Biashara ya thamani ya Dola za Marekani Bilioni Moja kwa mwaka.
Kwa upande wake, Mhe. James Millya (Mb.) ameishukuru Serikali ya Uturuki kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Sekta mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo Utali, Usafirishaji, Afya, Elimu na Uwekezaji huku pamoja na mambo mengine akibainisha kuwa ongezeko la safari za moja kwa moja za ndege kutoka Dares Salam, Kilimanjaro na Zanzibar kwenda Uturuki zinazofanywa na za Shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines) zimepelekea ongezeko kubwa la watalii nchini ikizingatiwa kuwa ndege hizo pia zina sehemu maalum inayojikita katika utangazaji wa vivutio vya utalii vinavyopatika nchini Tanzania.
Tanzania na Uturuki zilisaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara mwaka 2010 a Mkataba wa Kukuza na Kulinda Uwekezaji mwaka 2011, ambao ulianza kutekelezwa rasmi mwaka 2022, hatua iliyoongeza imani ya wawekezaji wa Uturuki nchini. Hatua hiyo imeiwezesha Uturuki kuwekeza kiasi kikubwa nchini katika sekta ya ujenzi, usafirishaji, viwanda na utalii, kwa wekezaji wa takribani dola za Marekani milioni 414.23 katika Tanzania Bara kupitia miradi 106 iliyotoa ajira 6,062, na dola milioni 96.4 Zanzibar kupitia miradi 12 ya utalii iliyotoa ajira 719 kwa wananchi.








