SAKATA LA SHEIKH PONDA NA BAKWATA LACHUKUA SURA MPYA
Dar es salaam - Sakata linalomhusisha na Kiongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limechukua sura mpya, baada ya viongozi wa dini kutoa kauli kali wakimtaka aheshimu taasisi hiyo inayotambuliwa kisheria kama chombo halali cha Waislamu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya sakata hilo Sheikh Said Mwaipopo amemtaka Sheikh Ponda kuliheshimu BAKWATA pamoja na uongozi wake, akisisitiza kuwa Sheikh Zuber ndiye kiongozi halali wa Waislamu Tanzania. Amesema BAKWATA ni taasisi inayotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo, kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa.
Sheikh Mwaipopo ameeleza kuwa Baraza hilo linafanya kazi zake kwa weledi na uimara, hivyo amemtaka Sheikh Ponda kuacha vitendo vya chokochoko na kauli zinazolenga kuchafua taasisi hiyo. Aidha, amesisitiza kuwa si sahihi kulinganisha BAKWATA na vyombo vingine vya kiimani, akieleza kuwa kila dini ina misingi, imani na madhehebu yake, hivyo kitendo hicho kinaweza kuleta uchonganishi miongoni mwa Waislamu.
Katika kauli yake, amemuelezea Mufti wa Tanzania kuwa ni kiigizo na kiunganishi muhimu cha umoja wa Waislamu nchini, na kwamba anapaswa kupewa nafasi ya kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa au kudhalilishwa.
Vilevile, Sheikh Mwaipopo amemtaka Sheikh Ponda kuacha kutumia masuala ya dini kama njia ya kutafuta huruma ya Watanzania, akidai kuwa anafanya hivyo baada ya kushindwa katika harakati za kisiasa, hususan za ubunge. Amesema vitendo hivyo vinachangia kuvuruga umoja wa Waislamu na Watanzania kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Sheikh Mwaipopo amelaani vikali madai ya Sheikh Ponda kushirikiana na watu wanaodaiwa kutokuwa na nia njema kwa Taifa, akimtuhumu kuuchafua Uislamu kwa kupokea hongo ili kuwavuruga Waislamu.
Amewataka Waislamu nchini kushikamana, kudumisha umoja na kuepuka kupeleka masuala ya kiimani mahakamani kwa lengo la kuvunja mshikamano wao. Pia amewahimiza Watanzania kwa ujumla kutozitumia imani za dini kama nyenzo ya kuwagawa waumini, bali wajenge misingi ya kupendana, kuvumiliana na kuitunza amani iliyopo nchini.
"Nitoe wito kwa viongozi wa wa pande zote zinazohusika kutumia busara, hekima na mazungumzo ya ndani ili kutatua tofauti zao kwa maslahi mapana ya umoja wa Waislamu na amani ya Taifa" Alisema sheikh Mwaipopo.




