Breaking News

ACT - WAZALENDO YAIBUA MAPUNGUFU KATIKA BAJETI KUU YA SERIKALI 2026/27

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Bi Dorothy Semu, amesema Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/27 imeshindwa kutoa majibu ya msingi kwa changamoto zinazowakabili Watanzania katika sekta muhimu za afya, kilimo na biashara.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha uchambuzi wa bajeti hiyo, Semu alisema kuwa Watanzania walitarajia kuona utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa na Serikali kuhusu kuboresha huduma za afya, hususan mpango wa afya kwa wote, lakini hali halisi inaonesha kuwa gharama za matibabu zinaendelea kuwa mzigo mkubwa kwa wananchi.

Alieleza kuwa gharama za vipimo na matibabu ya magonjwa sugu zimeendelea kuwa kubwa katika hospitali za umma, huku wananchi wakilazimika kulipia huduma ambazo awali zilitarajiwa kutolewa kwa urahisi zaidi. Kwa mujibu wake, bajeti hiyo haijaeleza namna itakavyopunguza gharama hizo wala kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote.

Bi Semu alihoji utekelezaji wa mfumo wa bima ya afya kwa wote, akidai kuwa mfumo uliopo haujafanikiwa kuwafikia wananchi wengi kama ilivyokusudiwa. Alisema takwimu zinaonesha kuwa idadi kubwa ya Watanzania bado hawapo katika mfumo wowote wa bima ya afya, jambo linalowalazimu kutumia fedha nyingi wanapougua.

Kwa mujibu wa ACT-Wazalendo, suluhisho la kudumu ni kuanzishwa kwa mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wote ambao utawezesha wananchi wote kuchangia kwa viwango vinavyolingana na uwezo wao, huku Serikali ikiwachangia wale wasiokuwa na uwezo wa kuchangia.

Katika sekta ya afya, Semu pia alieleza kuwa bado kuna uhaba mkubwa wa watumishi wa afya, dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma. Alisema bajeti ya mwaka 2026/27 haijaonesha mkakati wa kutosha wa kuajiri watumishi wapya wala kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu kwa wananchi.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Semu alisema wakulima wanaendelea kukabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za mbolea pamoja na utegemezi mkubwa wa mbolea kutoka nje ya nchi. Alidai kuwa zaidi ya asilimia 69 ya mbolea inayotumika nchini inaagizwa kutoka nje, hali inayochangia kupanda kwa gharama za uzalishaji.

Alisema bajeti hiyo haijaweka mikakati ya kutosha ya kuimarisha uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi ili kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje na kuwasaidia wakulima kupata pembejeo kwa bei nafuu.

Aidha, Semu alieleza kuwa sekta ya kilimo imeendelea kutengewa fedha chache ukilinganisha na mahitaji yake, licha ya kuwa ndiyo sekta inayoajiri idadi kubwa ya Watanzania na kuchangia sehemu kubwa ya pato la taifa. Alibainisha kuwa fedha zinazotengwa mara nyingi hazipelekwi kwa kiwango kilichoidhinishwa, jambo linalozorotesha maendeleo ya sekta hiyo.

Kuhusu Bandari ya Dar es Salaam, kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo alisema bado kuna maswali mengi kuhusu matokeo ya uwekezaji uliofanywa pamoja na ushiriki wa kampuni ya DP World katika uendeshaji wa bandari hiyo.

Alisema licha ya Serikali kueleza kuwa kiwango cha mizigo inayopita bandarini kimeongezeka, bado kuna changamoto za ucheleweshaji wa mizigo, uhaba wa miundombinu na kuendelea kuwepo kwa msongamano wa shughuli zinazohusiana na usafirishaji wa makontena ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

ACT-Wazalendo pia imeitaka Serikali kuweka wazi mikataba ya uendeshaji wa bandari pamoja na faida halisi inayopatikana kutokana na uwekezaji huo ili wananchi waweze kujua manufaa yanayopatikana kutokana na rasilimali zao.

Kwa ujumla, Semu alisema Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 imeendelea kuongeza mzigo kwa wananchi wa kawaida kupitia kodi na tozo mbalimbali bila kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto za msingi zinazowakabili.

Alisisitiza kuwa ACT-Wazalendo itaendelea kupigania matumizi bora ya fedha za umma na kusukuma sera zitakazohakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha Watanzania wote, hususan katika sekta za afya, kilimo, ajira na maendeleo ya uchumi.