TMA YABAINISHA NJIA RASMI ZINAZOTUMIKA KATIKA USAMBAZAJI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.
Zanzibar - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imebainisha njia rasmi zinazotumika katika usambazaji wa taarifa za hali ya hewa nchini, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari vilivyorasimishwa, tovuti ya Mamlaka pamoja na mitandao ya kijamii.
Akizungumza na wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Ofisi ya Zanzibar, Ndg. Masoud Makame Faki, alisema kuwa lengo la mazungumzo hayo ni kuwakaribisha wananchi kutembelea banda la TMA katika Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (ZITF) yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Nyamanzi kuanzia tarehe 29 Disemba 2025 hadi 16 Januari 2026.
Ndg. Faki aliwasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa kupitia njia rasmi zinazotumika na TMA, ikiwemo vyombo vya habari vilivyorasimishwa, blogu na tovuti ya Mamlaka (www.meteo.go.tz), pamoja na mitandao ya kijamii ya TMA ikiwemo YouTube, Instagram, Twitter, WhatsApp Channel na Facebook, ambazo akaunti zake zinapatikana moja kwa moja katika ukurasa wa mwanzo wa tovuti ya Mamlaka.
Aidha, aliwataka wananchi kuachana na tabia ya kusambaza taarifa potofu wanazozipata mitandaoni, akisema kuwa taarifa hizo zinaweza kuathiri mipango ya maendeleo inayoratibiwa nchini. Badala yake, aliwahimiza kufuatilia na kutumia taarifa sahihi za hali ya hewa zinazotolewa kupitia njia rasmi zilizobainishwa na TMA.
Kupitia maonesho hayo, TMA imeendelea kutoa elimu na ufafanuzi kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya hali ya hewa, ikiwemo hali ya fukuto la joto linaloendelea kujitokeza visiwani Zanzibar. Ndg. Faki alieleza kuwa kwa sasa Dunia inaendelea na mzunguko wake kuelekea katika kizio cha kusini, hali inayosababisha jua la utosi na hivyo kuongezeka kwa joto.
Aliongeza kuwa kutokana na Zanzibar kuzungukwa na maji, hali hiyo husababisha unyevu mwingi angani, jambo linalochangia wananchi kukumbwa na fukuto la joto linaloendelea kushuhudiwa katika kipindi hiki.








