Breaking News

WAZEE WATAKA KATIBA MPYA, MARIDHIANO YA KITAIFA

Dar es Salaam - Baraza la Wazee limeitaka Serikali kuanzisha upya mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likisema hatua hiyo ni muhimu katika kurejesha amani, mshikamano na maridhiano ya kitaifa baada ya matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Tamko hilo limetolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Mzee Joseph Butiku, kwa niaba ya Wazee waliokutana kujadili hali ya nchi.

Alisema wazee wameendelea kusikitishwa na matukio ya vifo, utekaji, kupotea kwa wananchi pamoja na uharibifu wa mali, wakisema matukio hayo yamesababisha hofu kubwa na kuathiri umoja wa kitaifa.

"Ni muhimu kwa Serikali kutoa taarifa kwa uwazi kuhusu yaliyojitokeza na matokeo ya uchunguzi unaoendelea, huku akitoa wito kwa wananchi kuwa na subira". Alisema Mzee Butiku 
Baraza hilo pia limeishauri Serikali kutoa fidia na msaada wa kisaikolojia kwa familia zilizoathirika kama hatua ya awali ya uponyaji wa kitaifa.

Kuhusu Katiba, Wazee wamehimiza utekelezaji wa ahadi ya Rais ya kuanzisha mchakato huru, wazi na jumuishi, utakaohusisha vyama vya siasa na makundi yote ya kijamii, na hatimaye kuhitimishwa kwa kura ya maoni.

“Katiba ni Sheria Mama na dira ya taifa. Ushiriki wa wananchi ni msingi wa uhalali wake,” 
Wazee pia wamependekeza kuundwa kwa Tume huru ya Maridhiano itakayoongozwa na mtu mwadilifu asiyeegemea upande wowote wa kisiasa, ikiwa na wajumbe wenye hekima na uzalendo.

Katika tamko hilo, Serikali imehimizwa kuendelea kusimamia haki, ikiwemo kutumia taratibu za kisheria kuwaachia huru mahabusu na wafungwa waliokamatwa kwa misingi ya kisiasa.
Wakati huohuo, Baraza la Wazee limeonya dhidi ya matumizi ya lugha ya matusi, chuki na uchochezi wa kidini au kikabila, likisema vitendo hivyo vinahatarisha amani ya nchi.

Wakigusia changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, Wazee wamesisitiza kuwa suluhu haipatikani kwa vurugu au kuifanya nchi isitawalike, bali kupitia mazungumzo na maridhiano ya kweli.

Tamko hilo limehitimishwa kwa wito kwa Watanzania kuweka maslahi ya taifa mbele ya maslahi binafsi au ya vyama, huku Wazee wakimwomba Mungu kuendelea kuibariki Tanzania.