WAZEE WASHAURI KUIMARISHWA AMANI, UMOJA NA HAKI NCHINI
Dar es Salaam — Wazee Wakongwe wa Taifa, chini ya uraghibishi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation (MNF), wamekutana jijini Dar es Salaam na kutoa maazimio mazito yanayolenga kuimarisha amani, umoja na haki nchini kufuatia matukio ya vurugu yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 22 Januari 2026 katika Ukumbi wa MNF, yakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa MNF, Mzee Joseph W. Butiku yamewakutanisha wazee kutoka mikoa ya dar, tanga, bukoba na Zanzibar.
Akisoma maazimio hayo kwa niaba ya Wazee, Mratibu wa Programu wa MNF, Dkt. Musuto Chirangi, alisema Wazee wamesikitishwa kwa kiasi kikubwa na uvunjifu wa amani uliosababisha vifo, uharibifu wa mali na miundombinu, pamoja na matukio ya watu kutekwa, kupotea au kuuawa, hali iliyozua hofu miongoni mwa wananchi na kudhoofisha mshikamano wa Taifa.
Wazee wametoa pole kwa familia zote zilizoathirika na kuwataka wananchi kuwa watulivu na wenye subira wakati Tume ya Uchunguzi ikiendelea na kazi yake.
Wamesisitiza umuhimu wa Serikali kutoa taarifa kamili, wazi na kwa wakati kuhusu vifo, uharibifu wa mali na hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya watakaobainika kuvunja sheria. Pia wamependekeza kuwepo kwa utaratibu wa kutoa pole, fidia, pamoja na misaada ya kiafya na kisaikolojia kwa waathirika.
Kuhusu masuala ya kikatiba, Wazee wametoa wito wa kuhuishwa kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna jumuishi, huru na wazi, ukihusisha vyama vya siasa na makundi yote ya wananchi. Wamesisitiza mchakato huo uwe na ratiba ya wazi itakayohitimishwa kwa kura ya maoni (referendum), sambamba na pendekezo la kutenganisha mamlaka na shughuli za Serikali na vyama vya siasa.
Katika eneo la uzalendo, haki na uwajibikaji, Wazee wamehimiza kila Mtanzania kuweka maslahi ya Taifa mbele ya maslahi binafsi, ya kichama au ya makundi. Wamesisitiza kuwa hakuna aliye juu ya sheria, haki itetewwe bila kuvunja sheria, na amani ilindwe bila kuuza haki. Vilevile, wameitaka Serikali kuimarisha usimamizi wa haki na usawa wa raia wote, ikiwemo kuachia huru kwa mujibu wa sheria wafungwa au mahabusu waliokamatwa kwa sababu za kisiasa, na kuendeleza uwazi katika usimamizi wa rasilimali na mifumo ya uwajibikaji.
Wazee pia wamewahimiza Watanzania kupenda bidhaa za ndani na kuamini wataalamu wa Kitanzania katika kutatua changamoto za Taifa, wakikumbusha wosia wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, kuhusu hatari ya kutegemea nguvu za nje katika kusuluhisha matatizo ya ndani.
Kuhusu ujenzi wa amani, utatuzi wa migogoro na maridhiano, Wazee wametambua changamoto ya ukosefu wa ajira na kipato duni, hususani kwa vijana. Wamesisitiza wajibu wa wazazi na viongozi kuwalea vijana katika misingi ya uzalendo, nidhamu na busara, huku wakishauri Serikali kuboresha sera za ajira, mitaala ya elimu na kupanua sekta zinazozalisha ajira.
Aidha, wazee hao wameonya juu ya matumizi ya lugha chafu, matusi na maandamano ya vurugu, wakisisitiza mazungumzo, usuluhishi na maridhiano ya kweli kuwa ndiyo njia sahihi ya kutatua migogoro ya kijamii na kisiasa.
Katika hatua nyingine Wazee wamependekeza kuundwa kwa Tume ya Maridhiano itakayojumuisha wajumbe wenye hekima, uadilifu na uzalendo wa dhati, ikiongozwa na raia asiye kiongozi wa upande wowote wa kisiasa, pamoja na kuwepo kwa maelezo ya wazi kuhusu aina na mwelekeo wa maridhiano hayo.
Pia wametoa wito na kukemea vikali matamko na vitendo vya kibaguzi vya aina yoyote, ikiwemo ubaguzi wa kidini, kisiasa, kikabila, kijinsia, kirika au kiuchumi.
Katika hitimisho lao, Wazee wamewahimiza Watanzania kuwajibika na kuwawajibisha wasiowajibika kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, kuweka maslahi ya Taifa juu ya ubinafsi, vyama au makundi, na kushirikiana kwa umoja katika kutatua changamoto na migogoro kwa amani.
“Tunaamini Watanzania hatujapoteza uwezo wa kuzungumza kwa uhuru, kwa busara na kwa umoja ili kujenga Taifa lenye amani, haki na mshikamano,” imesema taarifa hiyo.








