NGOME YA WANAWAKE YA ACT-WAZALENDO KUADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE KWA MAOMBOLEZO
.Dar Es Salaam -Ngome ya Wanawake ya ACT-Wazalendo imetangaza kuwa itaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu kwa maombolezo, kufuatia vifo na majeruhi waliopata ulemavu wa kudumu wakati wa ghasia zilizotokea Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 26, 2026 katika Makao Makuu ya chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake, Janeth Rite, amesema hawana sababu ya kusherehekea siku hiyo kwa sherehe ilhali mioyo ya Watanzania bado inalia kutokana na kupoteza wapendwa wao, huku wengine wakibaki na ulemavu wa kudumu.
Amesema mwezi Machi utakuwa mwezi wa maombolezo kwa wanachama na wafuasi wa ngome hiyo, wakionesha mshikamano na familia zilizoathirika na matukio hayo.
Kwa mujibu wa Rite, Machi 8, 2026 siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani watashiriki katika maombi na hitma, pamoja na kutembelea wazee na watoto yatima. Pia watafanya usafi katika vituo vya afya, kutoa misaada mbalimbali, kuchangia damu, kuzuru makaburi na kufanya mikutano mikubwa ya hadhara nchi nzima.
Amesema kauli mbiu yao mwaka huu ni, “Machozi ya Mama ni Deni la Taifa,” akisisitiza kuwa Ngome ya Wanawake ya ACT-Wazalendo itaendelea kuwa sauti ya wasiojiweza na haitanyamaza hadi haki itakapotendeka.
Rite amehitimisha kwa kutoa wito kwa jamii kushiriki kwa namna moja au nyingine katika maadhimisho hayo ya maombolezo, akisisitiza mshikamano, upendo na uwajibikaji wa kitaifa katika kipindi hiki kigumu




