RC CHALAMILA ARIDHISHWA NA UWEKEZAJI WA AFYA NA ELIMU KINONDONI
Dar es Salaam - Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameendelea na ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Kinondoni leo Februari 12, 2026, ambapo amekagua miradi ya maendeleo katika sekta za afya na elimu.
Katika ziara hiyo, RC Chalamila ametembelea Hospitali ya Shifaa iliyopo Hananasifu, Kinondoni, na kujionea huduma zinazotolewa na sekta binafsi katika utoaji wa huduma za afya. Ameeleza kuridhishwa na kiwango cha uwekezaji kilichofanyika hospitalini hapo na kusisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, RC Chalamila amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya uwekezaji na kuweka mazingira rafiki yatakayowavutia wawekezaji binafsi, kwa maslahi mapana ya wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amekagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Ghorofa ya Tarimba Abbas, yenye vyumba 21 vya madarasa, maktaba moja, vyumba vitatu vya maabara, jengo la utawala, maabara ya kompyuta pamoja na matundu 44 ya vyoo. Ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kupongeza juhudi zilizofanyika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
RC Chalamila amesisitiza kuwa maendeleo hayana chama, akibainisha kuwa lengo kuu ni kuwahudumia wananchi bila kujali itikadi zao. Katika hatua hiyo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika katika sekta mbalimbali nchini, hususan elimu.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa katika Wilaya ya Kinondoni inatarajiwa kuchukua siku tatu, ikilenga kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kesho, Februari 13, 2026, anatarajiwa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika eneo la Nyakasangwe, ambapo amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuwasilisha changamoto zao na kupata majawabu papo hapo.












