Breaking News

WAZIRI KAIRUKI: UWEKEZAJI KATIKA ANGA NA SATELLITE WAONGEZA KASI YA UCHUMI WA TAIFA

Dar es Salaam - Tanzania inatambua kuwa anga na matumizi ya Teknolojia ya Satelaiti ni msingi muhimu katika miundombinu ya mawasiliano unaolenga kuboresha maendeleo ya kidijitali, ujumuishaji wa kikanda na uimarishaji wa usalama wa mawasiliano.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Pamoja la Satelaiti la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliyofanyika tarehe 16 Februari, 2026 jijini Dar es Salaam.

Waziri Kairuki alibainisha kuwa Tanzania imenufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) ambao umewezesha kuunganisha nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Msumbiji na Zambia pamoja na ujenzi wa zaidi ya minara 2,151 ya mawasiliano kote chini ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Aliongeza kuwa, hatua hizo zimeongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini hadi kufikia asilimia 98.6 kwa 2G, 93.4 kwa 3G, 94.2 kwa 4G na 30.1 kwa 5G kufikia Desemba 2025.
Waziri Kairuki alieleza kuwa Tanzania inatekeleza Programu ya Taifa ya Anga (National Space Programme) ikiwemo Mradi wa KiboCube unaotekelezwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Anga ya Nje ya Dunia (UNOOSA) na Wakala wa Utafiti wa Anga wa Japan (JAXA). Mradi huo unalenga kujenga uwezo wa kitaalam wa wazawa na kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika teknolojia za satelaiti barani Afrika.

Mhe. Kairuki alisema kuwa Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa majadiliano hayo muhimu yanayolenga kuboresha matumizi ya teknolojia ya satelaiti yatakayosaidia sekta nyingine kama kilimo, madini, mazingira, usalama na udhibiti wa majanga hivyo kuongeza tija katika uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi.