ACT WAZALENDO YAZINDUA MNARA WA KUMBUKUMBU KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Dar es salaam - Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Chama cha ACT Wazalendo kupitia Ngome yake ya Wanawake kimezindua mnara wa kumbukumbu kwa ajili ya watu waliopoteza maisha kufuatia matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Uzinduzi huo umefanyika Machi 3, 2026, ambapo Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, alisema hatua hiyo inalenga kuenzi kumbukumbu ya waliopoteza maisha pamoja na kuonesha mshikamano kwa familia zilizoathirika.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dorothy alisema maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni fursa ya kutafakari nafasi ya wanawake katika jamii na changamoto wanazokumbana nazo, ikiwemo maumivu wanayopitia mama waliopoteza watoto wao katika matukio hayo.
“Machozi ya mama anayesubiri kurejeshewa mwili wa mwanae ni kilio kisicho na sauti, lakini chenye uzito mkubwa kwa taifa. Machozi ya mama ni deni la taifa,” alisema Dorothy.
Alisisitiza kuwa taifa linahitaji uponyaji wa kweli kufuatia matukio ya Oktoba 29, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kufikiwa kwa kukabiliana na ukweli wa yaliyotokea na kuhakikisha haki inapatikana kwa waathirika.
Aidha, alilaani vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyofanywa dhidi ya Watanzania na kusisitiza umuhimu wa kusikiliza sauti za waathirika badala ya kuficha ukweli.
Katika hatua nyingine, Dorothy alitoa wito wa kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi iliyo nje ya Serikali ili kuchunguza kwa kina matukio hayo, akisema ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha haki, uwajibikaji na maridhiano ya kweli kwa taifa.




