AL-HIKMA FOUNDATION KUGHARAMIA NDOA 130 KWA VIJANA WASIO NA UWEZO WA KULIPA MAHARI
Dar es Salaam - Taasisi ya Al-Hikma Foundation, waandaaji wa mashindano makubwa ya kuhifadhi Qur’an ya mabara mbalimbali, imetangaza mpango wa kugharamia mahari na kufanikisha ndoa 130 kwa vijana wasiokuwa na uwezo wa kifedha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Sheikh Nurdeen Kishk, amesema katika awamu ya mwaka huu utaratibu umebadilika ambapo mwanamke anayehitaji kuolewa ndiye atakayechukua fomu ya maombi kwa ajili ya mchumba wake ili kusaidiwa kulipiwa mahari.
Amesema fomu hizo zitatolewa kuanzia Machi 9 hadi Aprili 10 mwaka huu katika ofisi za Al-Hikma zilizopo Temeke, Dar es Salaam.
“Wanawake wanaotaka kuolewa katika awamu hii watakuja ofisini Al-Hikma kuchukua fomu kwa ajili ya wachumba wao. Fomu hizo zijazwe na kurejeshwa, kisha waombaji watasubiri hatua nyingine ikiwemo kufanyiwa usaili,” amesema Kishk.
Amefafanua kuwa hapo awali wanaume ndio waliokuwa wakichukua fomu hizo, ambazo zina masharti maalum yanayolenga kuhakikisha wanaoomba wanakidhi vigezo vya kusaidiwa kufunga ndoa, ikiwemo kuwa raia wa Tanzania.
Kishk amesema huu ni mwaka wa nne kwa Al-Hikma Foundation kuendesha mpango huo wa kusaidia vijana wa kike na wa kiume kufunga ndoa, ambapo hadi sasa taasisi hiyo imefanikisha ndoa 370.
Kwa mujibu wa Kishk, katika awamu ya mwaka huu taasisi hiyo imepanga kugharamia ndoa 130, huku Rais wa taasisi hiyo, Sheikh Sharif Al Ahadal, akiahidi kuongeza msaada wa ndoa nyingine 30.
Ameeleza kuwa miongoni mwa vigezo vya kuzingatiwa ni mwanaume kuwa na njia ya kupata kipato, kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka kwa Imamu wa msikiti anaoswali.
Masharti mengine ni pamoja na waombaji kuwa tayari wameposana, mwanamke awe anaolewa kama mke wa kwanza, na mwanaume asiwe na mke mwingine. Endapo mwanaume tayari ana mke na anataka kuongeza mke wa pili, atalazimika kugharamia mahari mwenyewe.
Aidha, waombaji wanatakiwa kukubali ndoa kufungwa jijini Dar es Salaam na kupata ridhaa ya wazazi wa mwanamke husika.




