LIPUMBA AAGA RASMI UENYEKITI CUF, ATOA WITO KWA UONGOZI MPYA KUIMARISHA CHAMA
Dar es Salaam — Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameuomba uongozi mpya wa chama hicho kuendelea kukijenga pamoja na kusimamia msimamo wa kudai kuundwa kwa Serikali ya mpito.
Akizungumza leo Machi 29, 2026 katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba alikabidhi rasmi ofisi kwa uongozi mpya unaoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Mirambo Camil Yusuph.
Katika hotuba yake, Profesa Lipumba alieleza kuwa licha ya kung’atuka kwenye nafasi hiyo, bado ana matumaini kuwa uongozi mpya utaendeleza juhudi za kuimarisha chama na kusimamia ajenda ya kudai katiba mpya itokanayo na maoni ya wananchi.
Alisema hali ya nchi inahitaji mabadiliko ya msingi, akigusia changamoto za ajira kwa vijana na kukata tamaa kunakoikumba jamii. “Ni muhimu kurejesha matumaini kwa wananchi kwa kuimarisha misingi ya demokrasia na utawala bora,” alisisitiza.
Hata hivyo, alieleza kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi wa chama uliofanyika Februari 21, 2026, akidai kuwa uliitishwa kufuatia maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, aliyedai uchaguzi wa Desemba 2024 haukufuata taratibu. Profesa Lipumba alitaja hatua hiyo kuwa ni “njama chafu” dhidi ya chama.
Aidha, alionya juu ya baadhi ya maamuzi ya kiuongozi ndani ya chama, akimtaja Hamad Masoud, akidai uteuzi wake kama Katibu Mkuu unazua maswali kutokana na kushindwa kusimamia baadhi ya majukumu muhimu hapo awali. Alisisitiza kuwa chama kinapaswa kuwa makini ili kuepuka kupoteza mwelekeo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya Mirambo Camil Yusuph alimshukuru Profesa Lipumba kwa mchango wake mkubwa ndani ya chama kwa zaidi ya miaka 26, akimtaja kama mwalimu na kiongozi mwenye uzoefu mkubwa wa kisiasa.
Alisema uongozi wake utazingatia misingi ya kidemokrasia kwa kuyawasilisha mapendekezo yote kwenye vikao vya chama kwa ajili ya majadiliano na maamuzi ya pamoja. “Tutaendelea kujenga umoja na mshikamano ili kufikia malengo ya chama, ikiwa ni pamoja na kushika dola,” alisema.
Bw. Yusuph alihitimisha kwa kuwataka wanachama wa CUF kuendelea kuwa wamoja licha ya changamoto za migogoro ya kiuongozi, akisisitiza kuwa migogoro hiyo si mipya bali ni sehemu ya safari ya chama, na inaweza kutatuliwa kwa mazungumzo na mshikamano.




