RC CHALAMILA ASHIRIKI IFTAR MAALUM ILIYOANDALIWA NA IKHSAN AID NETWORK
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameshiriki futari maalum iliyoandaliwa na Ikhsan Aid Network kwa ufadhili wa GSM Group na State Oil, yenye lengo la kuimarisha mshikamano wa kijamii bila kujali tofauti za kidini.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Msasani Tower, wilayani Kinondoni District, na imewakutanisha watu wa makundi mbalimbali, wakiwemo wenye mahitaji maalum, watoto kutoka vituo vya kulelea yatima pamoja na viongozi wa dini tofauti.
Akizungumza katika hafla hiyo, RC Chalamila amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kudumisha umoja, upendo na ushirikiano si tu katika kipindi cha Ramadhan bali wakati wote.
“Ni muhimu kuendeleza utamaduni wa kupendana na kusaidiana bila kujali dini zetu, kwani sisi sote ni Watanzania,” amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa matukio kama ya futari yana mchango mkubwa katika kuwakutanisha watu wa imani tofauti na kujenga uelewano, jambo linalosaidia kudumisha amani na utulivu nchini.
Hafla hiyo pia imelenga kuwasaidia na kuwajumuisha watu wenye uhitaji maalum, ikiwemo wenye matatizo ya kuona, pamoja na kuimarisha mahusiano ya kijamii kupitia mshikamano na ushirikiano baina ya jamii mbalimbali.











