Breaking News

VIJANA WATAKIWA KULINDA AMANI KWA MAENDELEO YA TAIFA

Jamii, hususan vijana, imehimizwa kuendelea kuthamini na kulinda amani iliyopo nchini ili kudumisha ustawi wa familia na taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na Sheikh Ramadhani Mzomizi, aliyesema kuwa machafuko yana athari kubwa kwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiroho, huku yakisababisha kuyumba kwa misingi ya familia.

Amesema familia ndiyo nguzo kuu ya maadili na mshikamano katika jamii, akisisitiza kuwa pasipo kuwepo kwa amani ndani ya familia, ni vigumu kufikia utulivu wa jamii na maendeleo endelevu.

Aidha, Sheikh Mzomizi amewataka wazazi kuwa mfano bora kwa watoto wao kwa kuonesha upendo, uvumilivu na hekima wanapokabiliana na changamoto za kifamilia. Ameonya dhidi ya migogoro isiyo ya lazima, akihimiza kujengwa kwa utamaduni wa kusameheana ili kuimarisha mahusiano ya kifamilia.

Katika hatua nyingine, ameitaka jamii kwa ujumla kuwa mabalozi wa amani kwa kueneza upendo na mshikamano miongoni mwa watu. Pia amesisitiza umuhimu wa kumtanguliza Mungu katika maisha ya kila siku ili kujenga msingi imara wa maadili utakaosaidia kudumisha amani ya kudumu.

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo umuhimu wa amani unaendelea kupewa kipaumbele katika juhudi za kuimarisha maendeleo ya taifa.