Breaking News

MARIDHIANO NA MAZUNGUMZO: NJIA PEKEE YA KUIVUSHA TANZANIA KUELEKEA SIASA ZA KISTAARABU

Kada maarufu wa chama cha CHAUMMA, Yericko Nyerere, ametoa mtazamo mzito kuhusu mwelekeo wa siasa nchini akisisitiza kuwa kwa sasa siasa za uanaharakati hazina tena nafasi, bali siasa za mazungumzo na maridhiano ndizo zinazohitajika kuivusha nchi.
 
Yericko anabainisha kuwa uanaharakati umekuwa adui mkubwa wa ustawi wa nchi na vyama vya siasa, akitolea mfano wa historia ya vyama vilivyowahi kufanya vyema kama NCCR-Mageuzi, CUF, na hata hali inayovikabili vyama kama CHADEMA kwa sasa. 

Anasema akizungumza katika mahojiano na moja ya televisheni za mtandaoni anasema kuwa vyama hivi vimejikuta vikipoteza nguvu na mwelekeo baada ya kuvamiwa na fikra za kiharakati ambazo zimesababisha wanasiasa halisi kuvihama vyama hivyo na kuviacha vikiwa havina siasa za kisayansi za kufanya, jambo linalovifanya vipoteze mvuto kwa umma.

Akifafanua kiini cha siasa halisi, Yericko anasema kuwa siasa ni hoja na siyo harakati za "nginjanginja" ambazo mara nyingi hupoteza mwelekeo pale mhusika anapogeuza madai yake kuwa lazima yatekelezwe bila kujali umuhimu wa kukaa kwenye meza ya mazungumzo. 

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, maridhiano ni mchakato wa kuwasilisha hoja na kusikiliza majibu ya upande wa pili, ambapo pande zote zinatakiwa kupeana muda wa utekelezaji badala ya kutaka kila kitu kimalizike kwa wakati mmoja. Anasema kuwa siasa za maridhiano siyo mfumo wa kugawana "mkate" au vyeo kwa siri, bali ni mchakato wa wazi wa kuwasilisha hoja na kujibiwa kwa hoja, huku kila upande ukitambua kuwa huwezi kupata kila kitu unachotaka kwa asilimia mia moja.

Yericko anasisitiza kuwa nguvu ya kweli ipo katika majadiliano kwani hata mataifa yaliyoendelea barani Ulaya hutatua migogoro yao ya kisiasa kupitia meza ya mazungumzo na mwishowe hukubaliana ili kuliwezesha taifa kusonga mbele. 

Ili kufikia maridhiano ya kweli, kuna haja ya kuwa na utamaduni wa kusikiliza hoja za chama tawala kama ambavyo upinzani unavyotaka usikilizwe, kwani kila upande una hoja za msingi za kwanini jambo fulani linatekelezeka au halitekelezeki kwa wakati husika. 

Anahitimisha kwa kusema kuwa msukumo wa mazungumzo ndio utakaofikisha Tanzania mahali pema, na kamwe siasa za uanaharakati ambazo hazina unyumbufu wa kibiashara na kisiasa haziwezi kuwa mwarobaini wa changamoto za nchi.