Breaking News

MIKOPO YA BILIONI 200 KWA VIJANA: ACT WAZALENDO YAHOJI UWAZI NA URATIBU WA SERIKALI

Dar es salaam - Ngome ya Vijana Taifa ya Chama cha ACT Wazalendo imeibuka hadharani kupinga utaratibu uliotumiwa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana katika usimamizi wa fedha za mikopo ya vijana zenye thamani ya shilingi bilioni 200.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Mei 8, 2026, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo, alisema kuwa chama hicho kilipinga tangu mwanzo uamuzi wa kupeleka fedha hizo katika wizara za kisekta badala ya kuwa na mfumo mmoja wa uratibu kupitia wizara husika ya vijana.

Kwa mujibu wa Nondo, hatua hiyo imechangia kukosekana kwa uwazi, uratibu na uwajibikaji katika mchakato mzima wa utoaji wa mikopo hiyo kwa vijana nchini.

Alisema hadi sasa hakuna taarifa za kutosha kutoka wizara za kisekta kuhusu namna fedha hizo zinavyotolewa au walengwa wake, jambo ambalo limeongeza mashaka juu ya usalama na matumizi ya fedha hizo.

“Jambo hili limepelekea kutokuwa na uratibu, uwajibikaji na uwazi kwa vijana. Ndiyo maana hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya kina kutoka wizara za kisekta kuhusu mikopo hii ya bilioni 200,” alisema Nondo.

Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo pia ilikosoa masharti yaliyowekwa na wizara kwa vijana waliotaka kuomba mikopo hiyo. Miongoni mwa masharti yaliyolalamikiwa ni hitaji la mwombaji kuwa na leseni ya biashara pamoja na vigezo vingine walivyodai kuwa vinawabagua vijana wengi wasiokuwa na uwezo wa kuanzisha taratibu hizo mapema.

Aidha, chama hicho kilieleza kutoridhishwa na muda mfupi uliotolewa kwa ajili ya maombi ya mikopo hiyo. Serikali ilitangaza rasmi dirisha la maombi Machi 21, 2026 na kulifunga Aprili 3, 2026, ikiwa ni siku 12 pekee.

Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, muda huo haukutosha kuwafikia vijana wengi kutokana na uhaba wa taarifa, ukosefu wa hamasa na changamoto za uratibu katika maeneo mbalimbali nchini. Nondo alisema mapendekezo yote yaliyotolewa na Ngome ya Vijana kuhusu kuongeza muda na kuboresha masharti yalipuuzwa na Serikali.

Alisema matokeo ya hali hiyo yalionekana wazi kupitia idadi ndogo ya vijana waliojitokeza kuomba mikopo hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, iliyomo kwenye kitabu cha bajeti ya wizara hiyo, vijana walioomba mikopo hiyo walikuwa 30,384 pekee.

Kutokana na hali hiyo, Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo iliamua kuhamasisha vijana kujitokeza kuomba mikopo hiyo huku baadhi ya viongozi wake wakiamua kuingia wenyewe kwenye mchakato wa maombi ili kufuatilia kwa karibu changamoto zilizopo.

Nondo alisema kupitia ushiriki huo wamefanikiwa kubaini dosari nyingi katika mfumo wa utoaji wa mikopo hiyo, jambo ambalo linaonesha haja ya Serikali kufanya maboresho makubwa ili kuhakikisha fedha za maendeleo ya vijana zinawanufaisha walengwa kwa haki, uwazi na usawa.

Kauli ya ACT Wazalendo inakuja wakati ambapo vijana wengi nchini wanaendelea kulalamikia ugumu wa kupata mitaji na mikopo ya kuanzisha au kukuza shughuli za kiuchumi, huku Serikali ikiendelea kusisitiza kuwa mfuko huo ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha vijana kiuchumi.