NJOMBE SHAMBA LA FEDHA, WAKULIMA WA PARACHICHI WAVUNA BILIONI 49
Mkoa wa Njombe umezidi kudhihirisha umahiri wake katika sekta ya kilimo ambapo katika msimu wa mwaka 2024/25, wakulima wa zao la parachichi wamefanikiwa kujipatia mapato ya jumla ya takribani shilingi bilioni 49.236 kupitia mauzo ya moja kwa moja.
Kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 31.2 zilitokana na tani 18,378.99 zilizouzwa nje ya nchi kwa bei ya wastani wa shilingi 1,700 kwa kilo, huku tani nyingine 29,986.77 zikiuzwa kwenye viwanda vya ndani ya mkoa kwa wastani wa shilingi 600 kwa kilo na kuingiza shilingi bilioni 17.9.
Takwimu hizo zimetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Njombe.
Alisema mafanikio haya yanachangiwa na uwepo wa viwanda vitano vya kuchakata parachichi vikiwemo AvoAfrica na Avodemia, vyenye uwezo wa kusaga tani 1,650 kwa siku, pamoja na vituo tisa vya kufungashia ambavyo vinahudumia pia mikoa jirani ya Mbeya, Iringa, Ruvuma, na Songwe.
Pia wakati akielezea mafanikio ya kilimo cha parachichi Msemaji wa Serikali alimtambulisha mkulima mwenye ekari 200 za zao hilo, aliyemtambulisha kwa jina moja la Msuya ambaye mwaka jana alifanikiwa kuuza matunda yake kwa Sh 3,700 kwa kilo kutokana na ubora wake. Wastani Wa mkoa kilo ni sh 1,700.
Alisema kwamba anapuzungumza kilimo kinalipa huyo ni mfano mojawapo kwani kutokana na kilimo chake cha kisasa aliweza kuvuna tani 200 alizopeleka sokoni kwa bei hiyo.
Amesema Serikali kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo na Benki ya Kilimo (TADB), imekuwa ikichagiza uwekezaji huu ambapo hadi sasa TADB imetoa mikopo ya thamani ya shilingi bilioni 173.11 katika kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao kama parachichi na viazi.




