RAIS DKT. SAMIA AHUTUBIA MKUTANO WA NISHATI YA NYUKLIA AFRIKA (NEISA 2026) UNAOFANYIKA NCHINI RWANDA
KIGALI, RWANDA - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amehutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kigali (Kigali Convention Center-KCC) Jijini Kigali nchini Rwanda, ambapo amezihimiza nchi za Afrika kuwekeza katika miradi ya kuzalisha umeme wa nyuklia utakao saidia kukuza uwekezaji katika Mataifa hayo.
Mkutano huo wa siku nne wa Kimataifa unawakutanisha pia wataalam wa nishati, wawekezaji na mashirika ya kimataifa, ambapo utajadili matumizi ya nishati ya nyuklia kwa maendeleo ya Bara la Afrika.
Aidha, utajadili namna bora ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme Afrika, kupunguza uchafuzi wa mazingira, kusaidia maendeleo ya viwanda, kukuza ubunifu wa teknolojia za nishati ya nyuklia pamoja na kuvutia wawekezaji katika miradi ya nishati.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ni miongoni mwa Mawaziri wa Tanzania walioambatana na Mheshimiwa Rais katika tukio hilo.
Mawaziri na Viongozi wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmood Thabiti Kombo, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri wa Maji Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Seif Kombo Pandu, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Felchesmi Mramba, Kaimu Naibu Katibu Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja wataalam kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC).




