RC CHALAMILA ATAKA WAKALA WA VIPIMO KUENDELEA KUTOA ELIMU YA UMUHIMU WA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameutaka Wakala wa Vipimo (WMA) kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu matumizi sahihi ya vipimo ili kuepusha matumizi ya vipimo batili vinavyoweza kuathiri haki za walaji nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani iliyofanyika katika Soko la Kariakoo, Chalamila amesema maadhimisho hayo yana umuhimu mkubwa katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya vipimo sahihi na madhara ya kutumia vipimo visivyo halali.
Amesema ni muhimu kwa Wakala wa Vipimo kushirikiana kwa karibu na wafanyabiashara ili kuhakikisha sera za usimamizi wa vipimo vya mizani, uuzaji wa mafuta pamoja na bidhaa nyingine zinazotumia vipimo zinafuatwa ipasavyo.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara kutambua kuwa matumizi ya vipimo batili ni dhuluma kwa wananchi na ni kinyume na maadili pamoja na mafundisho ya dini.
“Unapomtapeli mnunuzi kwa kutumia vipimo visivyo sahihi, unafanya dhambi kubwa mbele za Mungu na jamii. Vitabu vyote vya dini vinakemea vitendo hivyo,” amesema Chalamila.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa alikabidhi tuzo na zawadi kwa Soko la Kisutu baada ya kuibuka mshindi katika matumizi sahihi ya vipimo. Pia aliwataka wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kudumisha amani, kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi stahiki ili kusaidia juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za kijamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema haki hupatikana pale vipimo vinapotolewa kwa usawa, akieleza kuwa Serikali imeanzisha taasisi mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haki ikiwemo Wakala wa Vipimo.
Naye mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo, Francis Owelro, amesema vipimo vina mchango mkubwa katika shughuli za kila siku za biashara hivyo ni muhimu kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi vinavyokubalika kisheria.
Siku ya Vipimo Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Mei 20, ambapo kwa mwaka huu maadhimisho ya kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Dodoma yakiongozwa na kaulimbiu isemayo; “Sayansi ya Vipimo Hujenga Imani katika Uundaji wa Sera.”










