Breaking News

RIO FERDINAND ATUA NCHINI, ZIARA YAKE KUITANGAZA TANZANIA KIMICHEZO NA KITALII

Dar es salaam - Mamia ya wananchi leo Mei 19, 2026 walifurika katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, kumpokea nyota wa zamani wa soka duniani na nahodha wa zamani wa Klabu ya Manchester United pamoja na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand, aliyewasili nchini kwa ziara maalumu ya kimichezo na utalii.

Rio Ferdinand alipokelewa rasmi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, sambamba na viongozi mbalimbali wa michezo na wananchi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia ujio wake.
Ziara ya nyota huyo wa zamani wa soka nchini Tanzania inalenga kuhamasisha maendeleo ya michezo, hususan soka, pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa kama kitovu cha vivutio vya utalii. Ujio wa Rio Ferdinand unatajwa kuwa sehemu ya jitihada za kutumia michezo kama daraja la kuitangaza Tanzania duniani na kuvutia watalii zaidi kupitia ushawishi wa watu maarufu katika michezo.

Wananchi waliojitokeza katika mapokezi hayo walionekana wenye shauku kubwa ya kumuona na kumpokea mwanasoka huyo ambaye aliwahi kung’ara katika ligi kuu ya England na mashindano mbalimbali ya kimataifa akiwa mmoja wa mabeki bora duniani katika kipindi chake.
Katika ziara hiyo, Rio Ferdinand anatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii pamoja na kushiriki shughuli za kimichezo zitakazowakutanisha vijana na wadau wa soka nchini. Serikali imeeleza kuwa ujio wake ni fursa muhimu kwa Tanzania kuendelea kujitangaza kimataifa kupitia sekta ya michezo na utalii.