Breaking News

TMA NA EMEDO WATANGAZA TUZO ZA WANAHABARI KUHAMASISHA ELIMU YA HALI YA HEWA NA USALAMA MAJINI

Meneja Masoko na Uhusiano kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Bi. Monica Mutoni akitoa ufafanuzi kuhusu tuzo hizo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Mbezi Garden, Jijini Dar Es Salaam
Afisa Uchechemuzi (Advocacy Officer) kutoka Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo EMEDO, Bi. Mary Francis Mahemba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kuifikia jamii kwa taarifa sahihi uliofanyika katika ukumbi wa Mbezi Garden, Jijini Dar Es Salaam,



Dar es salaam - Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), leo wametangaza rasmi ushirikiano wa Tuzo za Waandishi wa Habari zinazolenga kuhamasisha elimu kuhusu hali ya hewa, tahadhari za mapema na usalama majini nchini Tanzania.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam, Afisa Uchechemuzi kutoka EMEDO, Bi. Mary Francis Mahemba, alisema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuifikia jamii kwa taarifa sahihi zinazosaidia kuokoa maisha, kupunguza athari za majanga yanayohusiana na hali mbaya ya hewa pamoja na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu usalama majini.

“Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu tahadhari za hali ya hewa, usalama majini na hatua za kujikinga dhidi ya majanga. Kupitia tuzo hizi tunatambua mchango wao katika kujenga jamii salama na yenye uelewa wa hatari za kuzama maji,” alisema Bi. Mahemba.

Tuzo hizo zinalenga kuhamasisha utayarishaji wa habari zenye ubora kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo matukio ya hali mbaya ya hewa na athari zake kwa jamii, tahadhari za mapema za hali ya hewa, usalama wa vyombo vya usafiri majini, uzuiaji wa ajali na vifo vitokanavyo na kuzama maji pamoja na ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga yanayohusiana na hali ya hewa.

Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizo zitawahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali nchini Tanzania.

Waandishi wa habari wamealikwa kuwasilisha kazi zao zilizochapishwa au kurushwa hewani ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 1, 2025 hadi Agosti 30, 2026. Kazi hizo zinapaswa kutumwa kupitia barua pepe za media@meteo.go.tz na mediahaliyahewa@gmail.com.

Kwa upande wake, Meneja Masoko na Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni, alisisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari za mapema katika kuokoa maisha ya wananchi, hususan wale wanaotegemea shughuli za maji kama vile uvuvi na usafiri wa majini.

Bi. Mutoni alisema TMA itaendelea kuhakikisha mchango wa wanahabari katika masuala ya hali ya hewa unatambuliwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuongeza thamani ya Tuzo za Wanahabari wa Masuala ya Hali ya Hewa nchini.

Ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma, mashirika ya kiraia na vyombo vya habari katika kuongeza uelewa, usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli za kiuchumi na kijamii.