VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUUNGANA KULIOMBEA TAIFA
Dar es salaam - Kiongozi wa dini, Sheikh Mwaipopo, amewataka viongozi wa dini nchini kuungana kwa pamoja, kuacha tofauti zilizopo katika jamii na kushirikiana kuliombea taifa ili kuendelea kudumisha amani na mshikamano wa Watanzania.
Akizungumza leo Mei 9, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao na viongozi mbalimbali wa dini, Sheikh Mwaipopo amesema kuwa kipindi hiki kinahitaji umoja mkubwa wa kitaifa na busara kutoka kwa viongozi wa kiroho, hasa katika kuhakikisha jamii inaendelea kuwa na utulivu na mshikamano.
Amesema viongozi wa dini wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri amani, upendo na maridhiano, huku akisisitiza umuhimu wa kujiepusha na makundi au mienendo yenye viashiria vya uvunjifu wa amani.
“Ni wajibu wetu kama viongozi wa dini kuwaunganisha wananchi na kulisemea taifa mema. Tusiwe sehemu ya migawanyiko, bali tuwe nguzo ya amani na mshikamano wa kitaifa,” amesema Sheikh Mwaipopo.
Aidha, amegusia hali ya kisiasa iliyojitokeza baada ya ripoti ya matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 2025, akieleza kuwa taifa linahitaji maombi na hekima zaidi ili kuendelea kulinda utulivu uliopo.
Katika hatua nyingine, Sheikh Mwaipopo amepongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na yenye amani.
Amesema juhudi za vyombo hivyo zimekuwa muhimu katika kuimarisha utulivu wa taifa na kuwafanya wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za kila siku kwa usalama.




