DC MTATIRO: AMANI NI CHACHU YA UWEKEZAJI NA MAENDELEO
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amesema utulivu na amani iliyopo nchini Tanzania imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali kuja kuwekeza katika miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.
Mtatiro ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea mradi wa maji uliotekelezwa katika Kijiji cha Zumve, Kata ya Nyamalogo, Wilaya ya Shinyanga. Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kulinda amani na kudumisha mazingira yanayowezesha maendeleo kupatikana.
Amesema wananchi wanapaswa kuwa raia wema kwa kutekeleza wajibu wao, kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na serikali pamoja na kuhoji kwa njia sahihi ili kuhakikisha serikali inatimiza wajibu wake kwa wananchi.
“Tunapoendelea kuwa wananchi wema, tukifanya kazi kwa bidii, kushirikiana na serikali yetu na kuihoji kwa njia sahihi ili itimize wajibu wake kwa wananchi, huku tukilinda amani yetu, tutaendelea kuvutia wawekezaji wengi zaidi,” amesema Mtatiro.
Aidha, amesisitiza kuwa wawekezaji hawawezi kupeleka mitaji yao katika nchi zenye migogoro na ukosefu wa utulivu, hivyo amani ni rasilimali muhimu inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania wakati wote.
“Hawawezi kupeleka uwekezaji kwenye nchi zenye migogoro. Amani ni jambo la msingi sana kwa maendeleo ya taifa letu, hivyo tuilinde mchana na usiku,” amesisitiza.
Mtatiro ameongeza kuwa ulinzi wa amani utaendelea kuvutia miradi mingi ya maendeleo kama mradi wa maji wa Zumve uliotekelezwa na shirika la Water for Good kwa kushirikiana na RUWASA, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi




