Breaking News

WATANZANIA WAASWA KUEPUKA UCHOCHEZI, VURUGU NA KULINDA AMANI YA TAIFA

Watanzania wameaswa kupuuza wito wa watu wanaohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani, wakielezwa kuwa vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha usalama, maendeleo na mshikamano wa taifa.

Rai hiyo ilitolewa Juni 4, 2026 jijini Dar es Salaam na mwanafalsafa wa Pan-Afrika kutoka Zimbabwe, Joshua Maponga, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa makala inayochambua matukio yaliyojitokeza kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Makala hiyo imeandaliwa na "africanspearhead.com" (https://reference-url-citation.invalid/1).

Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Maponga alisema baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yakipokea ufadhili kutoka nje kwa lengo la kuendesha shughuli zinazoweza kuathiri utulivu wa nchi na kuchochea migawanyiko katika jamii.

Kutokana na hali hiyo, aliiomba Serikali kufanya uhakiki wa mashirika hayo ili kubaini vyanzo vya fedha wanazopata pamoja na namna fedha hizo zinavyotumika.

Aidha, Dk. Maponga alieleza kuwa mara nyingi watu wanaohamasisha vurugu huendelea kuishi katika mazingira salama huku wananchi wanaoshiriki machafuko wakibeba athari kubwa, zikiwemo kupoteza maisha, mali na makazi.

Pia aliwataka waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda amani na athari za maandamano yanayogeuka vurugu, akisema kuwa matukio hayo yanaweza kudhoofisha maendeleo na kuathiri rasilimali za taifa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa "africanspearhead.com" (https://reference-url-citation.invalid/2), David Hundeyin, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye umuhimu mkubwa wa kiuchumi barani Afrika kutokana na nafasi yake ya kimkakati, hususan kupitia Bandari ya Dar es Salaam inayotumiwa na mataifa mbalimbali kwa shughuli za biashara na usafirishaji.

Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kulinda amani na rasilimali za nchi yao kwa kuwa machafuko yanaweza kusababisha athari kubwa za kiuchumi na kuchelewesha maendeleo ya taifa.

“Machafuko yana madhara makubwa kwa jamii na uchumi. Ni muhimu wananchi kuwa makini na taarifa au ujumbe wowote unaoweza kuchochea vurugu na kuhatarisha ustawi wa taifa,” alisema Hundeyin.