Breaking News

KANJEJERE WASTE MANAGEMENT YAONYESHA JINSI TAKA ZINAVYOWEZQ KUWA FURSA YA AJIRA NA NISHATI

Dar es salaam - Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajenjere Waste Management, Andrew Mathew, amesema taka si uchafu unaopaswa kutupwa tu bali ni rasilimali yenye uwezo wa kuzalisha ajira, mbolea, nishati na bidhaa nyingine zenye thamani kwa maendeleo ya jamii na uchumi wa taifa.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisno ya siku ya mazingira duniani mkoa wa dae es salaam, Mathew alisema kampuni hiyo imekuwa ikitumia teknolojia mbalimbali za kisasa kubadilisha taka kuwa bidhaa zenye manufaa, ikiwemo uzalishaji wa mbolea kwa kutumia viumbe maalumu wanaokula taka za kikaboni.

Alifafanua kuwa baada ya viumbe hao kutumia taka kama chakula, huzalishwa mbolea bora inayoweza kutumika katika shughuli za kilimo, hatua inayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza thamani ya taka.

Aidha, alisema kampuni hiyo imeanzisha mradi wa kuzalisha gesi kutokana na taka zinazokusanywa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono matumizi ya nishati mbadala na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati vinavyoathiri mazingira.

“Tumeamua kuonesha kuwa taka si kitu cha kutupa pekee. Kupitia ubunifu huu tunapata mbolea, gesi na hata malighafi za kutengeneza chakula cha kuku na mifugo,” alisema Mathew.

Kwa upande wa ajira, alisema sekta ya usimamizi wa taka imekuwa miongoni mwa sekta zinazotoa nafasi nyingi za ajira kwa wananchi wa makundi mbalimbali bila kujali kiwango cha elimu walichonacho.

Alisema kampuni hiyo imeajiri wahitimu wa vyuo vikuu, vijana wenye elimu ya msingi pamoja na watu ambao hawakupata fursa ya kusoma, mradi wawe na uwezo wa kufanya kazi na kufuata maelekezo.

Mathew pia aliipongeza serikali kwa kuendelea kushirikiana na wakandarasi wa usafi wa mazingira, huku akiomba kuwepo kwa mazingira bora zaidi yatakayowezesha kampuni za wazawa kuimarisha huduma na kuongeza ajira kwa wananchi.

Alisema usafi wa miji ni jambo muhimu hasa wakati Tanzania ikiendelea kujiandaa kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali katika matukio ya kimataifa na mashindano makubwa ya michezo yanayotarajiwa kufanyika barani Afrika.

Akizungumzia changamoto zilizopo, Mathew alitaja miundombinu pamoja na upatikanaji wa vifaa na magari ya kisasa kuwa baadhi ya maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na uchakataji wa taka.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa wananchi kutenganisha taka tangu majumbani kwao kwa kuweka taka za kikaboni, plastiki na makaratasi katika makundi tofauti ili kurahisisha mchakato wa urejelezaji na kuongeza thamani ya taka hizo.

Aliwataka waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa usimamizi sahihi wa taka na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Katika hatua nyingine, Mathew alisema tuzo mbalimbali ambazo kampuni hiyo imekuwa ikizipata zinatokana na ubunifu na mchango wake katika kuhifadhi mazingira pamoja na kuonesha namna taka zinavyoweza kubadilishwa kuwa fursa za kiuchumi.

Alisema mafanikio hayo yameiwezesha kampuni kushinda tuzo mbalimbali kwa zaidi ya miaka kumi mfululizo, huku ikiendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa taka na ulinzi wa mazingira.