Breaking News

MPOGOLO ATOA WITO WA UWAJIBIKAJI WA MAZINGIRA KWA TANZANIA YA KIJANI

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka viongozi, taasisi na wananchi kuongeza uwajibikaji katika utunzaji wa mazingira ili kufanikisha azma ya kuijenga Tanzania ya kijani na endelevu.

Mpogolo aliyasema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert John Chalamila, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Amesema kuwa pamoja na jitihada zinazoendelea kufanyika, Mkoa wa Dar es Salaam bado unakabiliwa na changamoto za ongezeko la taka ngumu, uchafuzi wa mito na bahari pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo wadau wote wanapaswa kushirikiana katika kutafuta suluhisho la kudumu.

Mpogolo amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za usafi wa miji, akibainisha kuwa ukuaji wa miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam unahitaji uwekezaji mkubwa zaidi wa vifaa vya kisasa vya usafi badala ya kutegemea mbinu za kawaida.

Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu ya “Dira ya Taifa 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania”, amesema kuwa Tanzania ya kijani inahitaji kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuongeza maeneo ya kijani, kutumia nishati safi na kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, amezitaka halmashauri kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi inazingatia maeneo ya kijani na kuimarisha utoaji wa elimu ya mazingira kuanzia ngazi za shule za msingi na sekondari ili kujenga kizazi kinachotambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Babu, amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kuwakumbusha wananchi wajibu wao wa kulinda mazingira kwani mazingira salama ndiyo msingi wa afya bora, uchumi imara na ustawi wa jamii.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vinavyochafua mazingira, kushiriki katika shughuli za usafi wa maeneo yao na kupanda miti ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhifadhi mazingira.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajenjere Waste Management, Andrew Mathew, amesema sekta ya usimamizi wa taka ngumu imeendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira kwa maelfu ya Watanzania pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Amesema taka hazipaswi kuonekana kama uchafu pekee bali kama rasilimali inayoweza kuzalisha ajira, mbolea, nishati na malighafi za viwandani.

Mathew amebainisha kuwa sekta hiyo imekuwa ikitoa fursa za ajira kwa watu wa kada mbalimbali, kuanzia wenye elimu ya juu hadi wasiokuwa na elimu rasmi, hivyo kuchangia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Aidha, ameiomba serikali kuendelea kuitambua sekta ya usimamizi wa taka kama sekta ya kimkakati kwa maendeleo ya taifa na kuangalia uwezekano wa kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwawezesha wakandarasi kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma.

Kuhusu maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, amesema wakandarasi wa taka ngumu mkoani Dar es Salaam wako tayari kushirikiana na serikali kuhakikisha jiji linakuwa safi, salama na lenye hadhi inayokidhi viwango vya kimataifa wakati wa mashindano hayo.

Maadhimisho ya mwaka huu yamewakutanisha viongozi wa serikali, taasisi za mazingira, halmashauri, sekta binafsi na wananchi kwa lengo la kutathmini mafanikio na changamoto za utunzaji wa mazingira pamoja na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kujenga Tanzania ya kijani.