MHE DKT JAFO AHITIMISHA MIAKA 29 YA PLAN INTERNATIONAL KISARAWE
KISARAWE - Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, leo amekuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufungaji wa shughuli za Plan International Wilaya ya Kisarawe, baada ya shirika hilo kutekeleza miradi ya maendeleo wilayani humo kwa miaka 29.
Dkt. Jafo ana historia ya kipekee na shirika hilo. Aliwahi kuwa Meneja wa Plan International Kisarawe kabla ya kuingia siasa na kuchaguliwa kuwa Mbunge.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dkt. Jafo aliwashukuru viongozi na watumishi wa Plan kwa mchango mkubwa katika maendeleo ya Kisarawe.
“Leo ni siku ya furaha kwangu. Nimepata nafasi ya kukutana tena na wenzangu tuliowahi kushirikiana kuwatumikia wananchi wa Kisarawe. Nawashukuru kwa mchango mkubwa nawatakia mafanikio mema huko mwendako,” alisema.
Wananchi bado wanamkumbuka Dkt. Jafo kwa usimamizi wake akiwa Meneja. Katika kipindi hicho alisimamia miradi mbalimbali ikiwemo: ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, miradi ya maji, madarasa, nyumba za walimu, ukarabati wa shule, madawati, matundu ya vyoo, na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Kisarawe.
Mkurugenzi Mkazi wa Plan International alimshukuru Dkt. Jafo kwa kazi kubwa aliyoifanya shirikani, akisema mchango wake umeacha alama kubwa Kisarawe. Pia alimpongeza kwa kuendelea kuwatumikia wananchi kwa ufanisi akiwa Mbunge.
Katika kutambua mchango huo, Dkt. Jafo alikabidhiwa zawadi mbalimbali kutoka kwa wadau na wawakilishi wa maeneo mbalimbali kama ishara ya shukrani.








