Breaking News

MWAMALANGA: KILA MTANZANIA AWAJIBIKE KULINDA AMANI

Na Mwandishi Wetu - Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini Tanzania, William Mwamalanga, ametoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika kulinda na kudumisha amani ya nchi, akisisitiza kuwa amani ni hitaji la msingi kwa kila mwananchi bila kujali tofauti za kisiasa, kijamii au kidini.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa amani nchini, Mwamalanga alisema viongozi wa dini na wadau mbalimbali wanaendelea na kampeni za kuhamasisha vijana kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha utulivu, mshikamano na maendeleo.

Alisema msimamo huo ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za viongozi wa dini katika kutetea amani, maadili mema na umoja wa kitaifa.

“Ushauri wetu kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ni kwamba kila Mtanzania awajibike kutunza amani. Sisi tupo kwenye kampeni ya kuhamasisha vijana kusitawisha amani katika kila eneo. Amani ni hitaji la kila mwananchi,” alisema Mwamalanga.

Alieleza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya amani na utulivu, huku akiwahimiza vijana kutumia nguvu na uwezo wao katika shughuli za maendeleo badala ya kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.

Aidha, alisema viongozi wa dini wataendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria, maadili na haki za wengine ili kuimarisha umoja wa Watanzania.

Mwamalanga alisisitiza kuwa jukumu la kulinda amani si la vyombo vya dola pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anachangia kwa maneno na matendo yanayojenga mshikamano na kuzuia migawanyiko katika jamii.

Kauli yake imekuja wakati ambapo viongozi mbalimbali wa dini na jamii wanaendelea kutoa wito wa kudumisha amani nchini, wakieleza kuwa ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.