Breaking News

WAZALISHAJI 20 WA MAZAO YA KILIMO IKOLOJIA WAJIFUNZA TEKNOLOJIA YA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO

Na Mwandishi Wetu - Wazalishaji 20 wa mazao ya kilimo ikolojia kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wamepata mafunzo ya teknolojia za kuongeza thamani ya mazao kupitia ziara ya mafunzo katika Kiwanda cha Intermech mkoani Morogoro, kinachojihusisha na utengenezaji wa mashine mbalimbali za uchakataji wa mazao ya kilimo.

Ziara hiyo iliratibiwa na Shirika la Island of Peace (IDP) kwa kushirikiana na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Mkoa wa Arusha (MVIWAARUSHA), chini ya Mradi wa ECO-FOOD unaolenga kuimarisha mifumo ya chakula endelevu kupitia kilimo ikolojia.

Washiriki wa ziara hiyo wamesema mafunzo waliyopata kuhusu matumizi ya teknolojia za uchakataji wa mazao yamewapa hamasa ya kuendeleza kilimo ikolojia pamoja na kuwekeza katika shughuli za kuongeza thamani ya mazao yao.
Kwa mujibu wa washiriki hao, mashine zinazotengenezwa na kutumika kiwandani hapo zina uwezo wa kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuboresha ubora wa bidhaa, kuimarisha vifungashio, kuongeza muda wa kuhifadhi bidhaa na hatimaye kuongeza thamani ya mazao pamoja na kipato cha mzalishaji.

Aidha, wameeleza kuwa uwekezaji katika teknolojia za uchakataji wa mazao una mchango mkubwa katika kufungua fursa za masoko, kuongeza ajira na kujenga mfumo wa chakula wenye tija na endelevu.

Mradi wa ECO-FOOD unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya IDP na MVIWAARUSHA ukiwa na lengo la kuimarisha uzalishaji wa mazao kwa njia za kilimo ikolojia, kuongeza thamani ya mazao na kuwawezesha wajasiriamali wanaoshiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa chakula.
Kupitia ushirikiano huo, washiriki wanaendelea kunufaika na mafunzo, kubadilishana uzoefu na kujengewa uwezo ili kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia uzalishaji, uchakataji na biashara ya mazao ya kilimo ikolojia.