Breaking News

POLISI TANZANIA YAONYA WANAOHAMASISHA UHALIFU KUPITIA MITANDAO YA KIJAMII

Jeshi la Polisi nchini limesema linafuatilia kwa karibu watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani na uhalifu vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa.

Akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa leo Juni 19, 2026, Msemaji wa Jeshi la Polisi na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime amesema baadhi ya watu wamekuwa wakihamasishana kufanya maandamano Julai 7 pamoja na kushawishi vitendo mbalimbali vya kihalifu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vitendo vinavyohamasishwa ni pamoja na kufunga barabara, kuchoma moto shule ili kusababisha taharuki kwa wazazi na walezi, kushambulia wananchi, kuua watu, kuharibu mali za umma na binafsi, pamoja na kuvamia askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kupora silaha na kuzitumia kutekeleza uhalifu.

DCP Misime amesema uhamasishaji wa vitendo hivyo chini ya kivuli cha maandamano haukubaliki kwa kuwa ni kinyume cha sheria za nchi, misingi ya utawala wa sheria pamoja na mikataba ya kikanda na kimataifa, na kwamba ni tishio kwa usalama wa taifa.

Amesisitiza kuwa hakuna haki inayoruhusu kuhamasisha vitendo vya uhalifu vinavyohatarisha maisha ya watu, mali zao na haki za wengine za kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kushirikiana kukataa na kupinga vitendo vyote vya kihalifu vinavyolenga kuvuruga amani, usalama na utulivu wa nchi. Aidha, wananchi wametakiwa kutosambaza ujumbe wowote unaohamasisha uhalifu, badala yake kutoa taarifa kwa vyombo husika ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Polisi imewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama nchini itaendelea kuwa shwari na kwamba itaendelea kulinda amani na utulivu kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wadau wengine wa usalama.