SERIKALI YAAGIZA WAFUGAJI WALIOSHINDA KESI WALIPWE FIDIA
Serikali imezielekeza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha wanawarejeshea haraka wafugaji mifugo yao au kuwapa fidia stahiki wale wote walioshinda kesi mahakamani baada ya kutaifishiwa mali zao.
Agizo hilo limetolewa leo bungeni jijini Dodoma wakati wa kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge ambalo limeahirishwa hadi Agosti 25, mwaka huu.
Hatua hiyo inakuja baada ya kubainika kuwa baadhi ya wafugaji katika maeneo mbalimbali walitaifishiwa mifugo yao baada ya kukamatwa kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, lakini baada ya kwenda mahakamani na kushinda mashauri hayo, taasisi husika zimeshindwa kutekeleza maamuzi ya kisheria.
Badala yake, taasisi hizo zimekuwa zikitoa sababu zisizo na tija kama vile kudai kuwa mifugo hiyo ilikufa au kupotea, jambo linalodhoofisha sekta ya mifugo na kuwaacha wananchi katika ufukara mkubwa.
Serikali imesisitiza kuwa kama mifugo hiyo ilikufa au kupotea, ni lazima wafugaji hao warejeshewe fidia kamili ya thamani ya mali zao ili kulinda misingi ya utawala wa kisheria na utoaji haki.
Ili kukomesha kabisa changamoto hiyo, Serikali imetangaza kuwa katika mkutano ujao wa Bunge, itawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria zinazosimamia utaifishaji wa mifugo na mali kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kwa lengo la kuifuta kabisa sheria hiyo.
Mbali na suala la mifugo, viongozi na watendaji nchini wametakiwa kuchapa kazi kwa bidii na kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku badala ya kupunguza kasi kwa kusubiri teuzi mpya, maarufu kama "mkeka" au "PDF".
Zipo taarifa zinazoonesha kuwa baadhi ya viongozi wamepigwa ganzi na kulegeza utendaji wakisubiri mabadiliko ya nafasi za uongozi, jambo linalosababisha huduma za umma kudorora.
Serikali imeonya kuwa watendaji wote watakaobainika kusubiri teuzi badala ya kuwahudumia wananchi wataondolewa mara moja na nafasi zao kuchukuliwa na watu wenye utayari wa kufanya kazi, kwani shughuli za umma hazitakiwi kusimama kwa sababu ya watu wachache wanaosubiri "mkeka".
Katika hatua nyingine, viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa wamekumbushwa kuwa utatuzi wa kero za wananchi ni jukumu lao la kila siku na hawapaswi kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa ili kutatua changamoto za msingi.
Ziara za viongozi wa ngazi za juu sio mbadala wa utendaji wa serikali za mitaa, hivyo wizara, idara, na sekretarieti za mikoa zimeelekezwa kuhakikisha mifumo ya kuanzia ngazi ya mtaa na kijiji inafanya kazi ipasavyo.
Taasisi zote zimetakiwa kutenga muda maalum wa kusikiliza changamoto za utoaji huduma, na viongozi wote watapimwa kwa namna wanavyotekeleza maagizo yanayotolewa.
Aidha Serikali imebainisha mpango wa kuondoa uchaguzi wa kila mwaka wa nafasi za Naibu Meya na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, ambao umekuwa ukigharimu fedha nyingi, kuchochea migongano, na kuzorotesha utulivu wa kiutendaji.
Katika mkutano ujao wa Bunge, yatawasilishwa mapendekezo ya kubadilisha mfumo huo ili viongozi wa nafasi hizo waweze kuongoza kwa kipindi chote cha uhai wa Baraza la Madiwani.
Marekebisho haya ya sheria yanatarajiwa kuleta utulivu wa kisiasa na kiutendaji, na kuwawezesha viongozi kujielekeza kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.




