Breaking News

SHEIKH JALALA: TUMUENZI IMAM HUSSEIN KWA KUDUMISHA AMANI, HAKI NA UMOJA

Dar es salaam - Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, amesema kumbukizi ya kuuawa kwa Imam Hussein (a.s.) ni fursa ya kuikumbusha jamii umuhimu wa kudumisha utu, haki, umoja na amani.

Akizungumza mara baada ya Matembezi ya Amani ya Kumuomboleza Imam Hussein (a.s.), mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliyeuawa katika vita vya Karbala, Sheikh Jalala alisema tukio hilo linafunza dunia juu ya madhara ya kuporomoka kwa maadili na haki.

Alitaja mambo matano muhimu yanayopatikana katika ujumbe wa Imam Hussein. Kwanza ni utu na ubinadamu, akisema kipindi hicho maadili hayo yalikuwa yamepotea hadi kufikia hatua ya mjukuu wa Mtume kuuawa mbele ya watu pamoja na familia yake kuteswa.
Pili, alisema Imam Hussein alisimama kuitetea haki wakati ambapo haki ilikuwa imeporomoka katika jamii. Alisisitiza kuwa haki inapaswa kutawala katika sekta zote za maisha.

Tatu, alieleza kuwa umoja wa Waislamu ulikuwa umesambaratika, hivyo akatoa wito kwa Waislamu wa madhehebu mbalimbali kuishi kwa mshikamano na kuacha migawanyiko.

Nne, alisema umoja wa kitaifa na wa dini mbalimbali ulikuwa umevurugika tofauti na kipindi cha Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ambapo watu wa dini tofauti waliishi kwa amani. Aliwataka Watanzania kuendelea kuuenzi umoja wa kitaifa.

Tano, alisema kuuawa kwa Imam Hussein ni ishara ya kupotea kwa amani na mshikamano katika jamii. Hivyo, aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Kwa upande wake, Mzee Azim Dewji alisema maombolezo hayo ni ujumbe wa kupinga dhuluma na ukandamizaji. Alisisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kusimama dhidi ya uonevu bila kutumia nguvu, wakimtegemea Mwenyezi Mungu.

Aliwataka wananchi kulinda amani na kuepuka tamaa ya kutafuta madaraka kwa nguvu, akisema uongozi ni amri ya Mwenyezi Mungu na haupaswi kupatikana kwa mabavu kwani huzaa madhara kwa taifa.
Naye Bi. Zainab Ndette alisema maadhimisho hayo yanalenga kueneza ujumbe wa kuitetea dini ya Mwenyezi Mungu, kusimamia haki na kupinga dhuluma.

Aliwataka Waislamu na watu wa dini zote kusimama imara kulinda amani, haki na mafundisho ya dini zao bila woga, akieleza kuwa Imam Hussein alitoa maisha yake kwa ajili ya kuilinda dini na kwamba ujumbe wake uliendelezwa na familia yake baada ya tukio la Karbala.

Alisisitiza kuwa jukumu la kila muumini ni kusimama na kuilinda dini pamoja na kuhubiri ukweli, haki na amani katika jamii.