Breaking News

WANAWAKE WAFANYABIASHARA: AMANI NI MSINGI WA BIASHARA ZETU

Baadhi ya wanawake wafanyabiashara wadogo wa mbogamboga katika Soko la Majengo, jijini Dodoma, wameeleza kuunga mkono uamuzi wa Serikali wa kusitisha mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, wakisema hatua hiyo itasaidia kudumisha amani na utulivu unaohitajika kwa maendeleo ya shughuli zao za biashara.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wafanyabiashara hao wamesema biashara ya mbogamboga hutegemea mwendelezo wa shughuli za kila siku, hivyo mazingira yenye amani na utulivu ni muhimu katika kuhakikisha wanaendelea kupata kipato na kulinda mitaji yao.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Winfrida, amesema uamuzi huo umeongeza matumaini kwa wafanyabiashara wadogo wanaouza bidhaa zinazoharibika kwa haraka, zikiwemo nyanya, mboga za majani na matunda, ambazo huweza kusababisha hasara kubwa endapo shughuli za biashara zitavurugika.

Amesema bado wanakumbuka athari zilizotokana na matukio ya Oktoba 29, ambapo wafanyabiashara wengi walipata hasara baada ya shughuli za biashara kusimama kwa muda, hali iliyoathiri uwezo wao wa kurejesha mikopo na kukidhi mahitaji ya familia.

Aidha, Winfrida amesema baadhi ya wafanyabiashara ni watu wenye changamoto za kiafya na ulemavu wanaotegemea biashara hizo kama chanzo kikuu cha kipato, hivyo amani na utulivu ni nguzo muhimu inayowawezesha kuendesha shughuli zao za kila siku bila vikwazo.