TANZANIA YAONGEZA JUHUDI KULINDA TAARIFA BINAFSI KUELEKEA UCHUMI WA KIDIJITALI WA DIRA 2050
Dar es salaam - Tanzania imeendelea kuchukua hatua muhimu katika kuimarisha usalama na ulinzi wa taarifa binafsi kadri matumizi ya teknolojia za kidijitali yanavyozidi kukua. Serikali imesisitiza kuwa ulinzi wa faragha ya wananchi ni msingi muhimu wa kujenga uchumi wa kidijitali unaoaminika, salama na jumuishi kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la Kwanza la Faragha na Ulinzi wa Taarifa Binafsi lililofanyika jijini Dar es Salaam, likiwa na kaulimbiu isemayo "Faragha ya Data kama Nguzo Kuu: Kulinda Mustakabali wa Kidijitali Jumuishi Kuelekea Dira ya 2050." Kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali kujadili mustakabali wa ulinzi wa taarifa binafsi nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Switbert Mkama, alisema taarifa binafsi ni nyenzo muhimu inayomtambulisha mtu, hivyo zinapaswa kulindwa kikamilifu ili kuhifadhi utu, haki na usalama wa wananchi katika mazingira ya kidijitali.
Alisema ukuaji wa huduma za mtandaoni na mifumo ya kidijitali umeongeza umuhimu wa kuwa na mfumo madhubuti wa kulinda taarifa binafsi. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilianzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) mwaka 2022 ili kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha uzingatiaji wa sheria hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkwilia, alisema kongamano hilo ni la kihistoria kwa kuwa ni la kwanza kufanyika tangu kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi mwaka 2022.
Alisema kongamano hilo linatoa fursa kwa wadau kutathmini mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa sheria hiyo, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuimarisha zaidi ulinzi wa taarifa binafsi nchini.
Dkt. Mkwilia alibainisha kuwa Tanzania inaendelea kushuhudia ongezeko kubwa la matumizi ya teknolojia na huduma za kidijitali, jambo linaloongeza ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi. Alisisitiza kuwa hali hiyo inahitaji mifumo imara ya usimamizi na ulinzi wa taarifa ili kulinda faragha ya wananchi na kuongeza imani katika matumizi ya huduma za kidijitali.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Dkt. Adadi Rajabu, alisema kongamano hilo ni hatua muhimu katika kujenga utamaduni wa uaminifu, uwajibikaji na haki katika matumizi ya taarifa binafsi.
Alieleza kuwa kuimarika kwa mifumo ya ulinzi wa taarifa kutasaidia kuongeza imani ya wananchi na wadau mbalimbali katika matumizi ya teknolojia za kidijitali, hatua ambayo itachochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kuifanya Tanzania kuwa na mazingira salama na shindani katika dunia ya teknolojia.







