WANNE MBARONI KWA TUHUMA MAUAJI YA MFANYABIASHARA RAIA WA CHINA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara raia wa China, Bhaozan Li, aliyekuwa mmiliki wa kiwanda cha kuchakata chupa cha XIL LI kilichopo eneo la Mabibo, Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na vyombo vya upelelezi vya Jeshi la Polisi kufuatia tukio hilo lililotokea Mei 16, 2026.
Alisema watuhumiwa hao walikiri kupanga na kutekeleza shambulio dhidi ya mfanyabiashara huyo usiku akiwa katika eneo la kiwanda chake, ambapo walimshambulia na kumuua kabla ya kuiba fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni tisa.
Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, baada ya kutekeleza tukio hilo watuhumiwa walitoroka na baadaye kukamatwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo Namanga mkoani Arusha na Mabibo jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Godson Simon maarufu kama Laizer (25), mkazi wa Olkolili, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro; Elisha Saitoti maarufu kama Luqmay (24), mkazi wa Mkonde, Handeni mkoani Tanga; Godfrey Laban maarufu kama Mollel (30), mkazi wa Makongo, Kinondoni; pamoja na Godson Pineli maarufu kama Lisika (24), mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam.
Kamanda Muliro amesema taratibu za kisheria zinaendelea na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za sheria.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu, likisisitiza kuwa vitendo hivyo huwasababishia wahusika madhara makubwa ya kisheria na kijamii.
Kwa sasa hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam imeelezwa kuwa ni shwari, huku shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi zikiendelea kama kawaida.




